Ripoti yataja changamoto za elimu Tanzania

Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga

Muktasari:

  • Ripoti ya haki za binadamu iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonyesha ufinyu wa bajeti, upungufu wa walimu, vyoo na madarasa ni kati ya changamoto zinazoathiri haki ya kupata elimu nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Ripoti ya haki za binadamu iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaonyesha ufinyu wa bajeti, upungufu wa walimu, vyoo na madarasa ni kati ya changamoto zinazoathiri haki ya kupata elimu nchini Tanzania.

Akizungumza leo Jumanne Agosti 20, 2019 mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga amesema hayo yamebainika katika ripoti ya nusu mwaka kuanzia Januari hadi Juni, 2019 iliyofanyika Tanzania Bara Tanzania.

Ripoti hiyo ilijikita katika vipengele kadhaa ikiwemo  uhuru wa kukusanyika, kujieleza, kujumuika, haki ya kuishi, kutobaguliwa, kuwa salama na uhuru dhidi ya ukatili.

Akisoma ripoti hiyo Henga amesema utekelezaji wa sera ya elimu bila ada umesaidia watoto wengi kufikia kupata elimu.

Amesema pamoja na utekelezaji huo, changamoto zilizojitokeza zinaathiri utoaji wa elimu kwa wanafunzi.

Naye mtafiti mwandamizi LHRC, Fundikira Wazambi amesema kuongezeka kwa ripoti za mimba za utotoni imekuwa kikwazo katika upatikanaji wa elimu ya mtoto wa kike.

“Matukio mengi ya mimba za utotoni yameripotiwa Tanzania Bara katika mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Lindi. Hii inafanya wasichana wengi waache masomo yao kwa sababu ya mimba,” amesema Wazambi.

Kuhusu afya, Henga amesema ufinyu wa bajeti na raslimali ndiyo changamoto walizobaini katika ripoti hiyo.

Hata hivyo, amesema Serikali imeendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha utekelezaji wa haki ya afya kulingana na raslimali zilizopo ikiwamo kujenga na kukarabati vituo vya afya katika sehemu mbalimbali nchini.