SINTOFAHAMU: Kinana, Makamba giza nene

Dar es Salaam. Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba wamekiweka katika mtego Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mjadala wa makatibu wakuu hao wa zamani wa chama tawala, umekiweka gizani kuhusu hatua ambazo zitachukuliwa dhidi yao au watakazozichukua wao kabla au baada ya kuhojiwa na kamati ya maadili.

Ukimya wa kitu gani kinachoendelea juu yao unazidisha mjadala ndani ya chama hicho, baada ya taarifa ambazo hakuna upande uliozithibitisha iwapo wamejiuzulu uanachama wa CCM na kupoteza sifa za kuhojiwa.

Taarifa za Kinana na Makamba kujiuzulu zimesambaa mitandaoni na Mwananchi limedokezwa kuwa barua zao za uamuzi huo wameziwasilisha ofisi ya katibu mkuu wa CCM zikiambatanishwa na kadi zao za uanachama.

Ingawa hakuna aliyekuwa tayari kuzungumzia uamuzi huo, iwapo Kinana na Makamba watafika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa leo, jitihada kubwa zitakuwa zimefanyika kuwashawishi.

Lakini habari zilizopatikana baadaye zilidokeza kuwa makada hao wamekubali kuhojiwa ama Dar es Salaam au Dodoma na baada ya hapo Kamati Kuu itakutana kujadili suala hilo.

CCM imekuwa na utaratibu wa kutumia watu wenye majina makubwa kushughulikia migogoro ya ndani inapoibuka kabla ya kusababisha mpasuko ndani ya chama hicho.

Kinana, Makamba na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe waliitwa mbele ya kamati ya maadili baada ya sauti zao kuenea katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto, uendeshaji nchi na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu hao dhidi ya mtu anayewachafua.

Membe alifika mbele ya kamati hiyo yenye wajumbe wanne Alhamisi iliyopita makao makuu ya CCM Dodoma, alihojiwa kwa zaidi ya saa 5 na baadaye akawaeleza waandishi wa habari jinsi alivyofurahishwa na mahojiano hayo na kuwa Mungu alimpa ujasiri wa kuzungumza kile alichotaka kuiambia kamati hiyo na hakuyumba wala kuyumbishwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Phillip Mangula akinukuliwa na gazeti la CCM akielezea jinsi wazee hao ambavyo wangehojiwa, alisema angefuatia Kinana kisha Makamba na wangemaliza kazi hiyo, wiki iliyopita.

Hata hivyo, Kinana na Makamba hawakufika kwenye kamati na hakuna taarifa zozote kuhusu kinachoendelea huku kujiuzulu kwao ndiyo mjadala unaotikisa kwa sasa hali inayokiweka katika wakati mgumu chama hicho tawala.

Wakati Kinana hakupatikana kuzungumzia suala hilo, Makamba alipopigiwa simu alisema, “Siko tayari kuzungumzia suala hili.”

Si Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally wala Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole aliyepatikana kuzungumzia suala hilo.

Lakini Mwananchi limedokezwa na mmoja wa wana CCM kuwa wazee hao wameona wachukue uamuzi huo ili kulinda heshima yao.

Msekwa na mchambuzi

Lakini Katibu wa Baraza la ushauri la viongozi wastaafu wa CCM, Pius Msekwa alipoulizwa jana na Mwananchi endapo ana taarifa za vigogo hao kuandika barua za kujiuzulu, alihoji, “Wamewasilisha kwa katibu mkuu au?

Kisha alisema endapo wameamua kujivua uanachama basi uamuzi wao unapaswa kuheshimiwa.

“Mmmh, ni vizuri. Ni watu wazima wana hiyari ya kufanya mambo kadiri wanavyoona inawafaa wao.

“Hata wewe una haki ya kufanya uamuzi unavyoona inakufaa, mtu mzima yeyote, kwa hiyo hilo halina mjadala,” alisema Msekwa aliyewahi kuwa Spika wa Bunge.

Msekwa ndiye aliyepokea barua za malalamiko ya Kinana na Makamba kuhusu kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi, uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Alipoulizwa endapo kuondoka kwao kunaweza kuleta dosari katika uhai wa chama hicho, Msekwa alisema chama hicho kina wanachama wengi.

“Kwa mfano chama kina wanachama zaidi ya milioni, mtu mmoja akiondoka kuna dosari gani? Au wawili wakiondoka, wewe vipi?” Alihoji huku akicheka.

Alisema hoja ya ushawishi ndani ya chama kwa kigezo cha nafasi na ukongwe wao kwa sasa haiwezi kuwa na madhara kwa kuwa walishastaafu.

“Hakuna ushawishi, mnaujenga nyinyi tu kwa mawazo yenu. Mimi nina ushawishi kwa sababu ya mambo ninayoyafanya sasa, wao wanasema ni wakulima wa nyanya huko Lushoto watakuwa na ushawishi gani? Makamba alisema msimuulize siasa, muulizeni kilimo, hamuheshimu hilo,” alihoji Msekwa aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM-Bara

Licha ya Msekwa kusema hayo, Kinana na Makamba walikuwa watendaji wakuu wa chama na wanajua siri na mtandao wa chama hicho.

Dk Muhidin Shangwe kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema mazingira ya njia panda kwa chama hicho yatajitokeza endapo watakuwa wamejiuzulu wenyewe kabla ya kuhojiwa.

“Hatumaanishi kwamba CCM itaondolewa madarakani, lakini ukweli ni kwamba lazima kutakuwa na athari kubwa, si makada wa kawaida hao kwa sababu kuna baadhi ndani ya chama wako upande wa Kinana na Makamba, halafu ni mazingira ya kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema Dk Shangwe.

“Pili, ni jaribio kwa CCM hata upinzani utachukua dosari hiyo na kuitumia kushawishi wananchi, lakini pia katika siasa ukijipanga hivi mwenzio anajipanga kwa namna nyingine, kama wamejivua uanachama itakuwa `timing’ (hesabu) mbaya kwa CCM, inawezekana hawakutegemea uamuzi wa Kinana na Makamba.”

Wakati Makamba alikuwa katibu mkuu mwaka 2007 hadi 2011, Kinana aliingia madarakani mwaka 2012 akichukua nafasi ya Wilson Mukama hadi Mei 29, mwaka 2018 alipomwachia Dk Bashiru, hivyo hata Serikali iliyoko madarakani ndiye alihusika kuiweka madarakani.

Kinana aliendesha kampeni ya kukirejesha CCM kwenye mstari baada ya kuzunguka nchi nzima kusikiliza na kutatua matatizo ya wananchi na wanachama, akiwa mkali kwa watendaji wa Serikali waliokuwa wazembe wakiwamo mawaziri aliowaita mizigo.

Ikiwa watakubali kuhojiwa, watakuwa na uwezekano wa kukutana na adhabu mbili kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la 2017.

Katika kanuni hizo kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi.

Kwa kuwa Kinana na Makamba si viongozi, watakapofika kwenye kamati hiyo ya Mangula watakuwa wakisubiri adhabu mbili ya kuwarekebisha na ikiwa itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama.

Makada wengine ambao sauti zao zilisikika katika mkanda huo ni Nape Nnauye, ambaye ni mbunge wa Mtama, William Ngeleja (Sengerema) na January Makamba (Bumbuli) ambao hata hivyo walimuomba radhi Rais John Magufuli na kusamehewa.

Sauti hizo zilizoanza kusambaa mitandaoni baada ya Kinana na Makamba kutoa waraka Julai 14 mwaka jana wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu ambaye amekuwa akiwadhalilisha na ambaye walimwelezea kuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Malalamiko yao waliyawasilisha kwa Msekwa na kuibua mjadala ndani na nje ya chama hicho.