Samia amtaka Zungu kusimamia muungano wa Tanzania, Zanzibar

Muktasari:

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemwambia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha muungano wa Tanzania na Zanzibar unaendelea kudumu.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemwambia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Azzan Zungu kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha muungano wa Tanzania na Zanzibar unaendelea kudumu.

Amemtaka Zungu ambaye ni mbunge wa Ilala kufanya ziara katika pande zote za muungano baada ya kuapishwa kuwa waziri wa wizara hiyo.

Samia ameeleza hayo leo Jumatatu Januari 27, 2020 Ikulu, Dar es Salaam baada ya Zungu kula kiapo.

Zungu aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa waziri wa wizara hiyo kuchukua nafasi ya George Simbachawene aliyehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kuchukua nafasi ya Kangi Lugola ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Samia amesema mwaka 2020 kuna kazi kubwa  kuhakikisha pande zote mbili za muungano chama tawala ninaibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

“Umezungumza vizuri kuhusu mazingira, na mara nyingi wateule huwa wanakwepa kuzungumza ya muungano, nataka nikwambie kuna changamoto  kubwa kwenye mambo ya muungano si kubwa sana kwamba upo hatarini hapana, ni mambo ya kufanyia kazi,” amesema Samia.

“Mimi mmoja leo nimetoa mmoja nimepokea mmoja, lakini nataka nikuhakikishie aliye toka tayari alikuwa anakwenda vizuri niliposikia umeninyang’anya nikauma kidole, lakini ni imani yangu kwamba  anayeingia atakuja kufanya kazi vizuri.”