Serikali ya Tanzania yatoa neno bei ya mahindi

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akijibu swali leo bungeni jijini Dodoma. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  •  Pamoja na kilio cha kila kona kwa wananchi kuhusu bei kubwa ya mahindi na unga, lakini Serikali imesema haitaingilia bei hiyo.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema licha ya bei ya mahindi kuwa juu, haitaingilia kupunguza bei kwani ni nafasi ya wakulima kupata bei wanayotaka.

Naibu Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Hussein Bashe ametangaza msimamo huo bungeni leo Jumatatu Novemba 11, 2019 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Busega (CCM), Dk Rafael Chegeni.

Mbunge huyo ametaka kujua ni hatua gani zinazochukuliwa na Serikali kuwasaidia Watanzania kupunguza mfumuko wa bei ambao sasa gunia la mahindi limefika bei ya Sh100,000.

Maeneo mengi nchini Tanzania kumekuwa na kilio kwa wananchi kuhusu kupanda kwa gharama za vyakula ikiwemo mahindi na unga.

"Mheshimiwa Spika, mwaka jana wabunge hapahapa walilalamika kuwa tunafunga mipaka ya uuzaji vyakula, leo bei imekuwa kubwa wanalalamika, sisi tunasema hatutaingilia bei ya vyakula bali bei ya ushindani ndiyo itapunguza gharama," amesema Bashe.

Naibu Waziri amesema kwa sasa kazi ya Serikali ni kuangalia maeneo ambayo yanashida kubwa ndipo wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula wanapeleka maeneo hayo kwa ajili ya kuuza kwa bei ndogo.

Bashe ametaka Watanzania kutumia ardhi iliyopo kwa ajili ya kuzalisha vyakula kwa wingi katika maeneo akisema ndiyo njia itakayopunguza bei ya mahindi sokoni.