Serikali ya Tanzania yaomba hukumu ya Sheikh Ponda kutenguliwa

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imeiomba Mahakama ya Rufani kutengua hukumu ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomhukumu kifungo cha nje katibu wa Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeiomba Mahakama ya Rufani kutengua hukumu ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomhukumu kifungo cha nje katibu wa Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda.

Maombi hayo yametolewa leo Jumanne Juni 11, 2019 na wakili wa Serikali mwandamizi, Nassoro Katuga kabla ya kuanza usikilizwaji wa rufaa ya Serikali kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomfutia Sheikh Ponda adhabu hiyo aliyohukumiwa na Mahakama ya Kisutu.

Mei 9, 2013 mahakama ya Kisutu katika hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi,  Victoria Nongwa, ilimpa adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja Sheikh Ponda kwa kosa la kuingia kijinai katika eneo la ardhi ya kampuni ya Agritanza Ltd, eneo la Chang’ombe Malkazi.

Sheikh Ponda akiwakilishwa na wakili,  Juma Nassoro alikata rufaa Mahakama Kuu na Novemba 27, 2014, Jaji Augustine Shangwa alimfutia adhabu hiyo, na Serikali kukata rufaa mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo.

Rufaa ya Serikali ilipangwa kusikilizwa leo na jopo la majaji watatu Stella Mugasha (kiongozi ), Ferdnand Wambali na Rehema Sameji.

Kabla ya kuanza usikilizwaji wakili Katuga ameieleza Mahakama wamebaini makosa ya kisheria kwa maelezo kuwa Mahakama ya Kisutu ilitoa adhabu hiyo bila kumtia hatiani.

Wakili Katuga ameiomba mahakama hiyo ibatilishe mwenendo wote wa Mahakama ya Kisutu kuanzia pale aliposomewa adhabu pamoja na wa Mahakama Kuu, kisha iiamuru Mahakama ya Kisutu imhukumu upya kwa kumtia hatiani kwanza kabla ya kumsomea adhabu.

Wakili Nassoro amekubaliana na hoja za wakili Katuga kuhusu kasoro hiyo ya kisheria lakini akaiomba mahakama ya Rufani iitupilie mbali hukumu hiyo ya Kisutu na kumwachia huru  Sheikh Ponda kwa madai kuwa hukumu hiyo ni batili badala ya kuamuru ahukumiwe upya.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote imesema kuwa itatoa uamuzi wake kwa tarehe ambayo itapangwa.