Serikali ya Tanzania yataja sababu kutowarejesha wanafunzi 420 waliopo China

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema haina mpango wa kuwarejesha nchini wanafunzi 420 waliopo mji wa Wuhan, nchini China kwa kuwa nchi zilizofanya hivyo zilisababisha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi husika.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema haina mpango wa kuwarejesha nchini wanafunzi 420 waliopo mji wa Wuhan, nchini China kwa kuwa nchi zilizofanya hivyo zilisababisha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi husika.

Imesema haiwezi kuwarejesha nchini kwa kuwa hakuna Mtanzania katika mji huo aliyepata maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana jioni Ijumaa Februari 14, 2020 inaeleza kuwa wanafunzi hao wapo katika mji ambao mlipuko wa ugonjwa huo ulianza, lakini hakuna aliyeugua hadi kufikia jana.

“Wizara inapenda kuuhakikishia umma kwamba Serikali ya Tanzania haina mpango wa kuwaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao waliopo Wuhan kwa kuwa wako katika uangalizi maalum nchini humo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inasema kuwa Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na  taarifa za kitabibu zinazobainisha kutokea kwa mlipuko wa maambukizi ya virusi hivyo katika mataifa ambayo awali yaliwaondoa wananchi wake China.

“Serikali itaendelea kufuatilia kwa ukaribu hali za Watanzania waliopo nchini China hususani katika jimbo la Hubei na mji wa Wuhan na kuchukua hatua kutatua changamoto zitakazojitokeza katika kipindi hiki,” inaeleza taarifa hiyo.

Tangu kubainika kwa virusi hivyo mwishoni mwa 2019 watu zaidi ya 1,000 wamefariki dunia.