Serikali ya Tanzania yatoa onyo watoroshaji madini

Muktasari:

 Serikali ya Tanzania imetoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na utoroshaji wa madini kwamba wakibainika hawatafumbiwa macho na hatua kali zitachukuliwa.

Geita. Serikali ya Tanzania imesema haitaona huruma kwa watu wachache watakaokamatwa wakijihusisha na utoroshaji wa madini na Serikali imejizatiti kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria

Akizungumza wakati wa kufungua maonyesho ya pili ya teknolojia ya madini leo Jumapili Septemba 22, 2019 mjini Geita, Majaliwa amewataka wanunuzi na wauzaji kutumia masoko ya dhahabu yaliyopo katika maeneo yao katika kufanya biashara ya madini

Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya madini na kuwalinda wawekezaji wanaofanya kazi za madini kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu husika.

Amesema kumekuwa na changamoto ya muda mrefu inayowakabili wachimbaji wadogo kwa kuchimba kwa kubahatisha huku wengine wakitumia imani za kimila kwa kukosa taarifa sahihi za kijiolojia.

Majaliwa amewataka wachimbaji wadogo kutumia taasisi ya jiolojia na utafiti wa madini nchini ili waweze kupata taarifa sahihi za wapi pa kuchimba na kupata madini.

Aidha amewataka kutumia maonyesho hayo kupata taarifa sahihi kwenye mabanda ya wizara ili waweze kuchimba kwa uhakika na faida na kuwataka wadau wa madini kuanzisha biashara za vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji hapa nchini.

Majaliwa amewataka wachimbaji wadogo kuepuka matumizi ya zebaki na kuanza kutumia njia mbadala zilizopo ili kupunguza madhara ya zebaki.