Serikali ya Tanzania yawataka maofisa habari kutumia mitandao ya kijamii

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akizungumza  Jijini Dodoma leo Disemba 2, 2019 wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya maofisa habari wa serikali  yaliyoandaliwa na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo. Picha Nazael Mkiramweni.

Muktasari:

Mafunzo ya siku tano ya maofisa habari wa Serikali yameanza leo Jumatatu jijini Dodoma yaliyoandaliwa na Chama cha Maofisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo.

Dodoma.  Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Juliana Shonza amewataka maofisa habari wa Serikali nchini humo kutopuuza mitandao ya kijamii badala yake waitumie kutangaza miradi mbalimbali inayofanywa katika maeneo yao na si kuwaacha wengine waisemee vibaya.

Shonza amesema hayo leo Jumatatu Desemba 2, 2019 wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya maofisa habari wa Serikali yanayofanyika jijini Dodoma yaliyoandaliwa na Chama cha Maofisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa kushirikiana na Idara ya Habari Maelezo.

Amesema mitandao hiyo ikitumiwa vizuri itasaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa haraka ili wajue Serikali yao inafanya nini katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2015/20.

Amesema kutokana na baadhi ya maofisa habari kutozungumzia yale yanayotekelezwa na Serikali ya Tanzania, imewafanya watu wengine kusema mabaya kuhusu Serikali katika jamii.

"Kuna changamoto ya maofisa habari kutotilia mkazo mitandao ya kijamii,  niwaambie kuwa msipuuze ina nguvu kupita kiasi, wenzetu waliofanikiwa wameitumia vyema  kutangaza yale ya wanayoyafanya na sisi tunatakiwa kufanya hivyo, " amesema Shonza

"Tunaenda kwenye uchaguzi mkuu 2020, tunaona Rais amefanya kazi kubwa ya kugusa maisha ya Watanzania, sasa ni kazi yetu sisi kuwajulisha wananchi ili waendelee kuwa na imani na serikali yao," ameongeza