Serikali ya Tanzania yawatoa hofu wateja iliyokuwa Benki ya FBME

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji

Muktasari:

Wizara ya Fedha na Mipango imesema taratibu za kuwalipa fidia wateja wa iliyokuwa Benki ya FBME ambayo ilifutiwa leseni yake nchini Tanzania inaendelea.

Dodoma. Jumla ya Sh2.404 bilioni zimelipwa kwa wateja 3,426 hadi Septemba 9, 2019 kama fidia ya bima amana kwa wateja wa iliyokuwa benki ya FBME ambayo iligutiwa usajili wake nchini Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi Septemba 12, 2019 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ambaye amesema kiasi hicho ni sawa na asilimia 55.9 ya kiasi chote kilichotarajiwa kulipwa kama fidia ya bima ya amana kwa wateja wote 6,628 waliopo Tanzania na walio nje ya Tanzania.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Jaku Hashim Ayub amehoji ni lini benki ya FBME italipa wateja amana zao ziliokuwepo kwenye benki hiyo na kuhoji benki iko katika hali gani huku akihoji Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina dhamana gani katika kulinda mabenki.

Naibu Waziri ameambia Bunge kuwa Sh2.401.2 bilioni zimelipwa ikiwa ni asilimia 83.3 ya lengo la kulipa Sh2,882.6 bilioni kwa wateja waliopo Tanzania tu.

"Wateja waliokuwa na amana zaidi ya Sh1.5 milioni watalipwa kiasi kilichobaki kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi lakini kwa wateja wenye amana zaidi ya kiasi hicho watalipwa kutegemea na ukusanyaji madeni na mauzo ya mali za benki," amesema Dk Kijaji.

Naibu Waziri amesema sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 inaipa Benki  Kuu ya Tanzania mamlaka ya kutoa leseni, kutunga kanuni, kusimamia benki zote zinazochukua amana za wateja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya benki zinazoendesha biashara.

Katika majibu ya nyongeza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelurdus Kilangi amesema hukumu iliyotolewa nchini Uingereza haina uhusiano na wala haitaathiri kitu chochote kwa wateja wa Tanzania.