Serikali yakiri bangi tatizo kubwa

Muktasari:

Licha ya kelele za baadhi ya wabunge kutaka kilimo na matumizi ya bangi yahalalishwe, Serikali imesema jambo hilo  ni gumu.

Dodoma.Serikali imesema licha ya kufanikiwa katika jitihada kubwa kwenye mapambano ya dawa za kulevya, bangi bado ni tatizo kubwa hasa katika mikoa ya Mara, Tanga, Morogoro, Arusha, Kagera na Ruvuma.

Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Jenister Mhagama ametoa kauli hiyo katika ukumbi wa habari wa Bunge leo Jumatano Novemba 6, wakati akizindua taarifa ya hali ya dawa za  kulevya ya mwaka 2018.

Mhagama amesema mapambano ya dawa za kulevya yanazidi kushika kasi na mafanikio yake ni makubwa kiasi cha kutia moyo na dunia imeridhika.

"Kwa mujibu wa shirika la Kimataifa la kupambana na dawa za kulevya na Uhalifu (UNODC), Tanzania ilipunguza uingizaji wa dawa za kukevya aina ya heroin kwa asilimia 90,"alisema Mhagama.

Waziri Mhagama amesema katika kipindi cha mwaka 2018 zilikamatwa tani 24.3 za bangi zikiwahusisha watuhumiwa 10,061 na mirungi tani 8.97  zikiwahusisha watuhumiwa 1,186.

Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, katika kipindi hicho jumla ya kesi 7,593 zikiwa na watuhumiwa 10,979 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini ambapo kesi 7,174 zilizowahusisha watuhumiwa 11,045 ziliendelea kusikilizwa.

Akijibu swali kuhusu madai ya baadhi ya wabunge kutaka bangi ihalalishwe, Waziri Mhagama amesema ni mchakato mrefu kufikia hatua hiyo lakini kwa sasa haiwezekani.

Mwisho,.....