VIDEO: Simbachawene agoma kufungua machinjio ya Msalato

Muktasari:

Miezi mitatu baada ya machinjio ya mnada maarufu wa Msalato mjini Dodoma kufungwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc),  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene amegoma kufungua tena machinjio hayo baada ya kubaini kasoro katika ukarabati

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),  George Simbachawene amegoma kufungua machinjio ya Msalato kutokana na kutoridhishwa na ukarabati uliofanyika.

Oktoba, 2019  Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) liliyafunga machinjio hayo yanayomilikiwa na Jiji la Dodoma na kuwatoza faini ya Sh5 milioni kwa uchafu.

Akizungumza leo Jumatano Januari 22, 2020  baada ya kutembelea machinjio hayo,  Simbachawene amesema jengo hilo lililokarabatiwa kwa Sh22 milioni halina viwango vya Serikali.

“Hili si jengo la Serikali ni la mlalahoi anaamua kujenga hivi lakini sio viwango vya Serikali. Sasa nikiuliza hela zilizotumika ni fedha za ajabu..., ninasema silifungui hao ng’ombe mchinjie mikononi haiwezekani jengo la serikali likawa ovyo namna hii,” amesema Simbachawene.

Kutokana na kutoridhika na ukarabati huo, waziri huyo ametoa wiki moja kwa  uongozi wa Jiji la Dodoma kufanya  marekebisho.