Simbachawene ataka polisi kutoa taarifa kwa maDC kila wanapofanya operesheni

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  George Simbachawene ameagiza kila operesheni itakayopangwa kufanywa na Jeshi la Polisi nchini taarifa zitolewe kwa mkuu wa wilaya husika.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,  George Simbachawene ameagiza kila operesheni itakayopangwa kufanywa na Jeshi la Polisi nchini taarifa zitolewe kwa mkuu wa wilaya husika.

Pia,  amepiga marufuku ukamataji wa wananchi, bodaboda na kufanya operesheni ya aina yoyote kwa kukurupuka hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani badala ya kujenga amani.

Akizungumza leo Ijumaa Februari 28, 2020 katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Simbachawene amesema ukamataji usio na mpangilio hauna tija na unaweza kuvunja amani badala ya kujenga.

 “Wananchi wanawalalamikia askari kukamata bodaboda bila sababu, hata kukamata kamata hovyo watu, ukamataji mwingine unakua kama kukomoana, hauna tija, hauleti amani, badala yake unasababisha amani itoweke.”

“Yaani msako fulani unatungwa hauna kichwa wala mguu, hauna maelekezo yoyote ya mkuu wa Polisi au chombo kingine, ni watu tu wanajitungia wanaondoka na pikipiki yao wamepakiana wanaenda kufanya operesheni ambayo haina utaratibu,” amesema.

Simbachawene amefafanua kuwa vyombo vya ulinzi na usalama ni vya wananchi, na operesheni yoyote haipaswi kufanyika bila mkuu wa Wilaya kupewa taarifa.

Ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Mpwapwa kwa kuwa karibu na wananchi kusikiliza kero zao na kuifanya Wilaya hiyo kuendelea kuwa na amani na utulivu.

Aliwataka viongozi wa Wilaya hiyo kujipanga vizuri katika maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa 2020.

Awali, mkuu wa polisi wa wilaya hiyo, Maulidi Manu amesema ujio wa Simbachawene umewasaidia zaidi kujipanga katika shughuli zao za kila siku.