Breaking News

Soka tamu la Chama lashtua

Sunday October 18 2020

 

By OLIVER ALBERT NA OLIPA ASSA

CLATOUS Chama kwa sasa yupo kwao Zambia kufuatilia pasipoti yake, kama ilivyo kwa beki Pascal Wawa aliyetimkia kwao Ivory Coast, lakini unaambiwa soka ambalo kiungo huyo amelionyesha tangu atue nchini limewashtua mpaka mastaa wa zamani wa klabu hiyo waliomchambua.

Chama alijiunga na Simba Julai, mwaka juzi na amekuwa chachu ya mafanikio ya kikosi cha Msimbazi kilichotwaa ubingwa misimu miwili mfululizo, kubeba Kombe la FA na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019.

Soka lake la kampa kampa tena, kumiliki mpira na zile pasi zake za visigino zimekuwa zikiwakosa wengi, kiasi cha wapinzani wao wa jadi, Yanga kumtamani awe katika kikosi chao, licha ya mwenyewe kusisitiza ataendelea kukipiga Msimbazi.

Katika ligi ya msimu huu Chama amehusika na mabao matano, akifunga mawili na kuasisti matatu na kuwafanya baadhi ya mastaa wa zamani wa Simba, Shekhan Rashid, Thomas Kipese na Amri Kiemba kudai kuwa kati ya nyota wa kigeni wa miaka ya karibuni jamaa katisha mbaya.

“Chama hatari sana yule mtu yaani miguu yake kama mikono. Anaweza kufanya chochote uwanjani ambacho kina msaada kwa timu yake.

“Anakupa burudani uwanjani, ana uwezo mkubwa wa kuamua matokeo ya timu yake. Ni mchezaji wa aina yake nashindwa hata nimuelezeeje ila katika sajili za hivi karibuni za Simba pale wamelamba dume. Hakunaga kama yeye kwa sasa”, alisema Shekhan aliyehamishia maskani nchini Sweden.

Advertisement

Winga aliyewahi kukipiga Yanga, Kipese alisema kati ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nchini, Chama ndiye anayemkuna kutokana na udambwidambwi alionao mguuni kwake, lakini kuwa msaada mkubwa kwa Simba.

Kipese alisema licha ya muonekano wa mwili wake kuwa mdogo, akili yake ya maamuzi ni kubwa yenye kuisaidia timu katika nyakati ngumu.

“Ni mchezaji ambaye hata wachezaji wenzake wanatakiwa kuiga mfano wake. Ujue anajua kuwakera watu uwanjani, mfano mtu unaenda kumkaba, anakuacha uende mwenyewe nyuma, yeye anaondoka na mpira, wakiwa kama sita ndani ya timu moja, basi kadi kwa wapinzani zitakuwa za kumwaga,” alisema.

Kwa upande wa Kiemba alisema Chama anatumia akili kubwa katika kazi yake kuisaidia timu kucheza kwa utulivu.

“Ndiye kiungo bora ninayemuona kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa, kwani anajipambanua katika majukumu yake, kumiliki mipira, kutoa pasi, kufunga vitu vyote hivyo anavyo,” alisema Kiemba..

“Aina ya uchezaji ule wachezaji wa timu pinzani wasipotumia akili kumkaba wanaweza wakawa wanasababisha faulo, kwani unaweza kuona anatoa mpira kwa mtu kumbe anakupiga chenga, unaenda nyuma yeye anasonga na mpira mbele kuwapa pasi washambuliaji.”

Advertisement