Spika Ndugai amkaribisha CAG Kichere bungeni

Monday November 4 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemkaribisha Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere na kumueleza kuwa yeye ni jicho la Taifa.

Ndugai ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 4, 2019 katika hafla ya kuapishwa kwa CAG iliyofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Spika huyo amemwambia kuwa taarifa yake inapowasilishwa bungeni, ni miongoni mwa taarifa muhimu, inapokelewa na wabunge na wanaichambua na kuijadili kwa umakini mkubwa.

“Tunakutegemea sana kama jicho letu, maana jicho ndiyo kila kitu kwa mwanadamu, bila jicho huwezi kujua unaelekea wapi, kwa hiyo wewe ni chombo muhimu sana kwa Taifa. Ni jicho la Taifa,” amesema Ndugai.

Amesema, “Kazi yako ni nzito sana ila nakuahidi kwa niaba ya Bunge, tutakusaidia na kukupa ushirikiano utakaohitaji na tunaamini imani ya mheshimiwa Rais kwako utailinda na kuitunza kama kiapo chako ulichokitoa hapa leo.”

Advertisement