Suti ya mbunge CCM yazua jambo bungeni, Ndugai atoa neno

Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Salum Mwinyi Rehani akiwasilisha bungeni taarifa za shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi.

Muktasari:

Spika Job Ndugai leo Jumatano Februari 5, 2020 amemtaka mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, Salum Rehani kubadili mavazi yake atakaporejea bungeni leo jioni.

Dodoma. Spika Job Ndugai leo Jumatano Februari 5, 2020 amemtaka mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, Salum Rehani kubadili mavazi yake atakaporejea bungeni leo jioni.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo mara baada ya Rehani ambaye ni mbunge wa Uzini (CCM) kumaliza kusoma taarifa ya kamati yake mbele ya Bunge, kubainisha kuwa alikuwa amevaa mavazi yaliyo chini ya kiwango kwa kamati hiyo muhimu.

Badala yake alimpongeza mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dastan Kitandula kuwa alikuwa amevaa mavazi mazuri.

"Waheshimiwa wabunge kamati kama hii ipo na nchi za wenzetu, sasa unapokuja kusoma halafu hujapiga vitu siyo sawasawa, nilitegemea uje umepiga vitu hapa, siyo kaunda suti, najua una vitu sasa jioni  uje umepiga ili uendane na kamati," amesema Ndugai.

Rehani alikuwa amevaa suti ya rangi ya bluu bahari yenye mikono mirefu lakini alipoelezwa kuwa jioni abadilishe vazi alisimama na  kugeukia alipoketi Ndugai na kuinama, akiashiria kuwa amekubaliana na agizo hilo.