TCU yatoa maagizo kwa wanafunzi waliochaguliwa chuo zaidi ya kimoja

Muktasari:

  • Zaidi ya wanafunzi 20,858 nchini Tanzania waliochaguliwa zaidi ya chuo kimoja wametakiwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuthibitisha udahili katika vyuo ambavyo ni chaguo huku dirisha la pili la maombi likifunguliwa.

Dar es Salaam. Wakati majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu Tanzania katika awamu ya kwanza yakitangazwa, wanafunzi 20,858 wamechaguliwa katika chuo zaidi ya kimoja.

Kutokana na hilo, wameamriwa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja kwa kutuma ujumbe mfupi wenye namba maalumu ya siri uliotumwa kupitia namba ya siri au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.

Hao yamebainishwa jana Jumatatu Agosti 26,2019 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Dk Kokuberwa Mollel kwa niaba ya Katibu Mtendaji, wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja wanatakiwa kuthibitisha udahili wao katika vyuo wanavyopenda kuanzia Agosti 20 hadi 29, 2019.

“Ili kupata namba ya siri, wanatakiwa kuingia katika mifumo ya udahili ya vyuo walivyochaguliwa kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalumu ya siri ili kuweza kujithibitisha,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo

“Uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti ya muombaji walizotumia wakati wa kuomba udahili kupitia vyuo husika,” imesema

Mbali na hilo, dirisha la awamu ya pili kwa udahili wa wanafunzi wa chuo kikuu lilifunguliwa tangu Agosti 21,2019 na linatarajiwa kufungwa Agosti 29, 2019.

Dirisha hilo limefunguliwa kutokana na baadhi ya waombaji kutochaguliwa katika awamu ya kwanza ya udahili, kutoa fursa kwa wahitimu walioshindwa kuomba mara ya kwanza, waliokuwa wamedahiliwa miaka ya nyuma na kukatisha masomo yao pamoja na wahitimu wa mitihani ya Cambridge mwaka 2019.