TMA watangaza mvua juu ya wastani Machi hadi Mei

Muktasari:

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetoa angalizo kuhusu kuwepo kwa mvua ya juu ya wastani katika eneo kubwa la nchi kati ya mwezi Machi mpaka Mei, 2020.

Dar es Salaam.  Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetoa angalizo kuhusu kuwepo kwa mvua ya juu ya wastani katika eneo kubwa la nchi kati ya mwezi Machi mpaka Mei, 2020.

Mkurugenzi wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema hayo leo Alhamisi Februari 13, 2020 wakati akizungumzia msimu wa mvua za masika zitakazoanza Machi mpaka Mei.

Amesema baadhi ya maeneo yatapata mvua ya juu ya wastani jambo linaloweza kusababisha maafa

na kuzitaka taasisi mbalimbali kuchukua tahadhari.

Mvua hizo zinatarajia kuanza kati ya wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi Machi na kumalizika kati ya wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi Mei.

"Tunazishauri taasisi zinazosimamia maafa kutoa taarifa kwa wakati kwa wakazi wanaoishi kwenye maeneo hatarishi ili wajiandae kukabiliana na mafuriko yanayoweza kusababisha uharibifu wa mazingira, miundombinu na kujaa maji," amesema Dk Kijazi.

Amesema mvua hizo zitayakumba zaidi maeneo ambayo hupata misimu miwili ya mvua na kwa wakulima, aliwataka kuandaa mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi.

"Lakini ni wakati wa kuvuna maji hivyo mamlaka husika zinaweza kutumia ipasavyo teknolojia ya uvunaji wa maji pia wadhibiti maji ya kunywa," amesema Dk Kijazi.

Kwenye sekta ya afya, Mkurugenzi huyo amesema kuna uwezekano mkubwa wa kutokea magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu hivyo mamlaka husika zichukue tahadhali.

Amewataka wavuvi kujenga tabia ya kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kila baada ya siku 10 ili wajihadhari na upepo mkali baharini.