TMA yatangaza mvua kubwa mikoa 10 Tanzania

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  (TMA) imetoa tahadhari kwa wakazi wanaoishi mabondeni katika mikoa kumi inayotarajiwa kunyesha mvua kubwa kuanzia leo Jumamosi hadi Jumapili ya Januari 12, 2020.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  (TMA) imetangaza uwezekano wa kutokea mvua kubwa kuanzia leo Ijumaa Januari 10, 2020 katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

Taarifa iliyotolewa na TMA mamlaka hiyo imesema uwezekano wa kutokea mvua hizo ni wa wastani na zinaweza kuambatana na athari.

Athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo ni pamoja na  makazi yaliyo maeneo ya mabondeni kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa siku ya kesho Jumamosi Januari 11, 2020 angalizo la mvua kubwa limetolewa katika mikoa Singida, Dodoma, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

Mvua hizo zitakazoendelea hadi siku ya Jumapili zinatabiriwa kuwa na athari na hata kusimamisha baadhi ya shughuli za kiuchumi.

Kufuatia hilo, TMA imewataka wakazi wa mikoa husika kuchukua tahadhari ili kuepusha kutokea kwa majanga yanayosababishwa na mvua kubwa.