TMA yatangaza ongezeko la joto Tanzania

Muktasari:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa juu ya kuwepo kwa hali ya ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo nchini, kufuatia kuwepo kwa kiwango kikubwa cha unyevunyevu angani kinachofikia asilimia 80 na zaidi katika baadhi ya maeneo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kutakua na ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo nchini humo, kufuatia kuwepo kwa hali ya unyevunyevu angani.

TMA imeyataja maeneo yatakayoathirika zaidi ni ukanda wa pwani yanayotarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha joto cha nyuzi joto 32 hadi 34 hususan kwa maeneo ya Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba.

Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumanne, Januari 7, 2020 na Mkurugenzi Mkuu TMA, Dk Agnes Kijazi imeeleza kwa kawaida kipindi cha Oktoba hadi Machi kila mwaka 2020 jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia.

Amesema Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine.

“Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya mwishoni mwa Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa),”

 

“Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine,” amesema Dk Kijazi.

Amesema nyakati za usiku pia kunaonekana kuwa na hali ya joto kutokana na kuwepo na kiwango kikubwa cha unyevunyevu angani kinachofika asilimia 80 na zaidi kwa baadhi ya maeneo.

Amesema unyevunyevu huo hutunza hali ya joto litokanalo mionzi ya jua na hivyo kuleta hali ya fukuto.

Mvua za vuli

Dk Kijazi amesema kwa sasa msimu wa mvua za vuli umeisha katika maeneo mengi hususan yale yaliyoko ukanda wa Pwani, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Simiyu, Shinyanga hivyo kuwa na joto kali.

“Pamoja na maeneo hayo mkoa wa Tabora nao unatarajiwa kuendelea kupata vipindi vya joto kali.”

Amesema katika wiki ya kwanza hadi ya tatu ya Januari 2020 viwango vya juu vya joto kwa baadhi ya maeneo yaliyopo ukanda wa pwani yanatarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha joto cha nyuzi joto 32 hadi 34 hususan kwa maeneo ya Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba.

“Vipindi hivi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kuongezeka zaidi Februari 2020 wakati jua litakuwa la utosi hapa nchini. Baada ya kipindi hicho hali ya joto inatarajiwa kuanza kupungua hasa kuelekea Machi ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka katika maeneo yanayopata mvua za msimu na kuanza kwa msimu wa mvua za masika.”

Hata hivyo, amesema taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika utabiri wa kila siku na TMA.