Takukuru wampa siku 10 mkandarasi kukamilisha mradi wa maji Dodoma

Wednesday December 4 2019

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma,  Sosthenes Kibwengo 

By Nazael Mkiramweni, Mwananchi [email protected]

Chemba.  Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma,  Sosthenes Kibwengo ametoa siku 10 kwa kampuni ya Juan kukamilisha mradi wa maji wa Kelema Kuu Wilaya ya Chemba.

Wakazi wa eneo hilo wanatumia maji ya bwawa ambayo si safi na salama huku wengine wakitembea umbali wa maili mbili hadi kijiji cha Kelema Balai kutafuta huduma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Desemba 4, 2019 baada ya kutembelea mradi huo, Kibwengo amesema awali kampuni hiyo ililazimika kununua mabomba ya Sh51 milioni kufidia gharama ya mradi huo wa Sh223 milioni.

Amesema mradi huo ulikamilika mwaka 2014 na kufanya kazi kwa wiki moja na mabomba yake kupasuka kutokana na kuzidiwa na presha ya maji kutoka katika kisima.

Amesema kampuni hiyo ilitakiwa kutumia gharama zake kununua vifaa vinavyokidhi mahitaji ya mradi huo.

“Hizi siku kumi tulizotoa kwa kampuni hiyo zinawatosha kukamilisha mradi huu ambao wametumia muda mrefu bila kuukamilisha na ukiangalia mvua zinakaribia kuanza.”

Advertisement

“Sasa katika kuepuka visingizio wanatakiwa kuukamilisha kabla siku hizo hazijaisha, na hakutakuwa na msamaha kwani ni uzembe na udanganyifu uliofanywa,” amesema Kibwengo.

Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) wilayani hapo, Robert Mganga amesema kazi iliyobaki ni nyepesi, kwamba  wiki moja inatosha kukamilisha kazi ya kutandaza mabomba akiahidi kuwasimamia kwa ukaribu ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliotolewa.

Mkurugenzi wa kampuni ya Juan, Innocent Benard amesema wakazi wa eneo hilo wategemee kupata maji muda wowote kwani watakamilisha mradi huo ndani ya muda uliotolewa.

Amesema mradi huo ungekamilika kwa wakati lakini ulicheleweshwa na walioagizwa kununua vifaa kufanya udanganyifu, kuwaomba wananchi kuwa na subira kwani wataanza kutumia maji hivi karibuni .

Advertisement