Takukuru yaokoa Sh86 bilioni tangu mwaka 2015

Muktasari:

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru) imeokoa Sh86 bilioni zilizotokana na ukwepaji kodi na makosa mbalimbali ya ufisadi tangu mwaka 2015.

Dodoma.  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (Takukuru) imeokoa Sh86 bilioni zilizotokana na ukwepaji kodi na makosa mbalimbali ya ufisadi tangu mwaka 2015.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Agosti 31, 2019 na msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Amesema kati ya fedha hizo,  Sh14.6 bilioni zimerudishwa serikalini kwa kuwa zimepatikana katika uhalifu.

Dk Abbas amesema Sh10 bilioni zimerudishwa serikalini baada ya kuuza magari, nyumba na vituo vya mafuta.

“Takukuru pia wamerejesha zaidi ya Sh25 bilioni, zikiwemo fedha zilizopatikana kwa rushwa baada ya washtakiwa kukutwa na hatia, fedha hizo zinarudi kwa Watanzania,” amesema Dk Abbas.

Amesema Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA)  imeokoa Sh46.8 bilioni zilizotokana na mikataba mibovu waliyoibaini wakati wa ukaguzi.

“Ipo mikataba waliyoikuta ikiwa tofauti yaani thamani ya fedha kwenye mkataba na kilicholipwa havifanani, mfano mtu alitakiwa kulipwa milioni moja analipwa milioni mbili,  fedha ya Serikali ziliyolipwa kimakosa lazima zitarejea serikalini ili zitumike kutekeleza miradi kwa wananchi,” amesema.