Takukuru yawaanika waliomuomba rushwa mfanyabiashara wa K’koo

Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Athuman Diwani

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewataja watumishi watatu wakiwemo askari polisi wa wili wa kituo cha Polisi cha Oysterbay Dar es salaam na mtumishi wa TRA Makao makuu kwa kosa la kuomba rushwa kwa mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe wa Kariakoo Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) leo Jumatatu Juni 10, 2019  imewataja askari polisi wawili na mtumishi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliohusika na ukamataji pamoja na uzuiaji wa mizigo wa mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe.

Takukuru imewataja watumishi hao ni Charity Ngalawa ambaye ni mwajiriwa wa TRA makao makuu, askari Polisi PC Simon Sungu pamoja na askari polisi PC Ramadhani  Uweza wote wakitokea kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Athuman Diwani imesema watumishi hao wanatuhumiwa kwa kosa la kuomba rushwa ya Sh2 milioni kutoka kwa mfanyabiashara huyo kinyume cha kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya 2007.

 “Uchunguzi wa Takukuru umebaini kwamba, watuhumiwa hao waliomba kiasi hicho cha fedha kama kishawishi ili waweze kuachia mzigo wa mfanyabiashara huyo ambao waliukamata kwa madai ya kufanya udanganyifu wa kiwango cha bidhaa na hivyo kuathiri ukadiriaji wa kodi,” imesema CP Diwani.

Taarifa hiyo pia imesema kuna watuhumiwa wengine waliohusika kwa namna moja au nyingine katika suala hilo bado wanachunguzwa.

Mbali na watuhumiwa hao, Takukuru pia inawashikilia watumishi wanne wa TRA Mkoa wa Ilala Dar es Salaam wakichunguzwa kwa ukaguzi na ukadiriaji wa kodi walioufanya kwa bidhaa za mfanyabiashara Dilesh Solank ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Sanaa ya Steps Entertainment.

“Watumishi hao wa TRA wanachunguzwa kwa kosa la kutumia madaraka yao vibaya kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya 2007 ambapo wanadaiwa kutoa makadirio ya juu ya Sh3.1 bilioni kama kodi za bidhaa za mfanyabiashara huyo jambo linaloshawishi rushwa,” imesema taarifa ya Takukuru.

Kamishna Diwani pia amezungumzia madai ya unyanyaswaji na madai ya rushwa kwa wafanyakazi wa kiwanda cha Tumbaku Morogoro (Tanzania Leaf Tobacco Company) yanayodaiwa kufanywa na Polisi mkoani Morogoro.

“Tayari Takukuru makao makuu imeiongezea nguvu timu ya uchunguzi mkoani Morogoro ambayo ilikuwa imeshaanza kazi chini ya usimamizi wa ofisi ya mkuu wa Takukuru Mkoa. Uchunguzi dhidi ya tuhuma hii utakapokamilika tutatoa taarifa kamili,” amesema Diwani

Diwani amewataka wananchi kuunga mkono Rais John  Magufuli katika mapambano ya rushwa na kuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani katika kesi zinazochunguzwa na Takukuru.