VIDEO: Tamwa: Wanawake wawezeshwe kushiriki chaguzi zijazo

Wednesday September 11 2019

 

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimevitaka vyama vya siasa, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla kuandaa mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki chaguzi zijazo.

Chaguzi hizo ni pamoja na ule wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.

Akizungumza na wahariri walipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata Relini jijini Dar es Salaam leo Septemba 11, 2019 Mwenyekiti wa Tamwa, Joyce Shebe aliyeambatana na Mkurugenzi wa chama hicho, Rose Ruben, amesema katika chaguzi hizo wanawake wanapaswa kuwa sehemu muhimu kwa hatua zote na sio katika kupiga kura pekee.

“Katika uchaguzi ujao ni vyema wanawake wapewe kipaumbele. Vyama vitoe fursa kwa wanawake kuwania uongozi, wasionekane katika kupiga kura tu,” amesema.

Kwa upande wake Rose alisema wanatarajia kuandaa mafunzo yatakayowahusisha wanawake wa kada mbalimbali ikiwamo waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa namna ya kuripoti na kutoa kipaumbele kwa wanawake katika uchaguzi ujao.

Msanifu Kurasa Mkuu wa Gazeti la Mwananchi, Angetila Hosia aliwahakikishia viongozi hao wa Tamwa kuwa MCL imeendelea kutoa kipaumbele katika mambo ya kijinsia.

Advertisement

Angetile alisema suala la kutoa kipaumbele kwa wanawake lipo katika sera za kampuni hiyo na kwamba inaendelea kusimamiwa na kutekelezwa kikamilifu.

Mbali na suala la kutoa kipaumbele katika habari zinaohusu wanawake, Rose aliwahamasisha waandishi wa habari wanawake kuendelea kujiunga na kukitumia chama hicho kwa kuwa ni jukwaa lao la kitaaluma.

Alisema Tamwa ina program tofauti zenye manufaa kwa waandishi wa habari wanawake ikiwamo inayohusu mikopo ya kujiendeleza kimasomo kwa wanawake wenye vigezo katika tasnia hiyo.

Joyce na Rose walikuwa katika ziara ya kujitambulisha na kuimarisha uhusiano wa chama hicho na MCL baada ya kuchaguliwa hivi karibuni kuisimamia na kuendesha Tamwa.

Advertisement