Tanesco waanza mchakato uwekaji umeme kwa mgonjwa anayepumulia mashine

Friday September 6 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mchakato wa kutenganisha mita atakayotumia mgonjwa anayeishi kwa kupumulia mashine Hamad Awadh (28) umeanza kwa mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kufika nyumbani kwa mgonjwa huyo na kufanya tathmini ya awali.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Septemba 6, 2019 Kaimu Meneja Mawasiliano Tanesco, Leila Muhaji amesema tayari mchakato wa kufunga umeme kwa ajili ya Awadh umeanza.

“Mafundi wetu wameenda pale na kuangalia namna gani watafanya, kuna vitu viwili vya kufanya kuna watu wa ‘estate’ walishaenda meneja wa viwandani wa Ilala alienda na mafundi na wakaangalia nini cha kufanya,” amesema Muhaji.

Kwa upande wake, Awadh amesema mafundi hao waliwasili saa nne asubuhi na kufanya tathmini namna ya kuiweka luku hiyo.

“Wamekuja na kuangalia namna umeme ulivyo hapa, wamechunguza na wameniambia watarudi Jumatatu kwa ajili ya kuifanya hiyo kazi,” amesema Awadhi.

Wakati huohuo, leo Ijumaa jopo la madaktari bingwa watano wa kifua, mapafu na magonjwa ya kuambukiza kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Chuo Kikuu cha Afya Shirikishi (MUHAS) limekutana na kufanya tathmini kuhusu tatizo linalomkabili Awadh na namna ya kulishughulikia.

Advertisement

 

Advertisement