Tanesco yawaomba radhi wakazi wa Kagera kukaa gizani kwa saa 24

Muktasari:

  • Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) limewaomba radhi wateja wake wa wilaya za Bukoba Mjini na Vijijini, Misenyi, Karagwe, Kyerwa na maeneo jirani kwa kukosa umeme kwa zaidi ya saa 24.

Dar es Salaam. Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) limewaomba radhi wateja wake wa Mkoa wa Kagera kutokana na kukatika kwa umeme mkoani huo tangu jana Jumatatu Agosti, 2019.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo leo Jumanne Agosti 20, 2019 inaeleza kuwa umeme ulikatika jana asubuhi baada ya kutokea hitilafu upande wa Uganda.

“Hitilafu hiyo imesababisha wilaya za Bukoba mjini na Vijijini, Misenyi, Karagwe, Kyerwa na maeneo jirani kukosa huduma ya umeme.”

“Maeneo yanayopata huduma ya umeme kwa sasa ni Wilaya za Ngara, Muleba na Biharamulo,” imeeleza taarifa hiyo iliyowekwa katika ukurasa wa rasmi wa shirika hilo katika mtandao wa Instagram leo saa 5 asubuhi.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hivi sasa wataalamu wa Shirika la Umeme la Uganda kwa kushirikiana na wataalamu wa Tanesco wanaendelea na kazi kuhakikisha huduma ya umeme inarejea.