Tanzania kufungua ofisi ya ubalozi Namibia

Muktasari:

  • Nchi za Tanzania na Namibia zimekubaliana kufungua balozi miongoni mwao ili kuimarisha uhusiano wa muda mrefu ulioanza tangu wakati wa mapambano ya kupigania uhuru kwa nchi zilizochelewa kupata uhuru.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Tanzania itafungua ubalozi wake nchini Namibia hivi karibuni ili kuimarisha uhusiano na Taifa hilo.

Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Jumatatu Desemba 2, 2019 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC), iliyokutana kwa mara ya pili leo tangu mwaka 1999 ilipokutana kwa mara ya kwanza.

Profesa Kabudi amesema Namibia nayo imetangaza kufungua ubalozi wake hapa nchini kutokana na shinikizo la wananchi wake ambao wametaka nchi hiyo iwe na ubalozi Tanzania, kutokana na historia ya ushirikiano baina ya mataifa haya.

“Wakati wa ziara ya Rais John Magufuli huko Namibia, alitangaza kwamba tutafungua ubalozi Namibia. Muda wowote kabla mwaka huu haujakwisha, balozi wetu atakwenda Namibia na Balozi wa Namibia naye atakuja kuanza kazi hapa,” amesema Profesa Kabudi.

Katika mkutano wa pili wa Tanzania na Namibia, nchi hizo zimetiliana saini hati ya makubaliano (MoU) kwenye maeneo mbalimbali yakiwamo ya sekta za utalii, madini, viwanda, biashara na kuwawezesha vijana.

Amesema Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Namibia hasa kwenye sekta ya utalii kwa sababu nchi hiyo inafanya vizuri kwenye sekta hiyo kutokana na kulitumia jangwa vizuri kuvutia watalii. Amesema wamewekeza pia kwenye sekta ya utalii.

Waziri huyo amebainisha kwamba, Namibia nayo ina mambo ya kujifunza kutoka Tanzania kama ya fani ya udaktari ambapo nchi hiyo imekuwa ikileta wanafunzi wake kuja kujifunza fani hiyo katika vyuo vya hapa Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwa amesema nchi yake inaishukuru Tanzania kwa mchango wake wakati wa kupigania ukombozi wa Taifa lake mpaka lilipopata uhuru mwaka 1990.

Amesisitiza kutekelezwa kwa makubaliano yaliyofikiwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili huku akitaka Tume hiyo kukutana mara kwa mara kuangalia utekelezaji wa makubaliano hayo.

“Tutafurahi kuona makubaliano haya yanatekelezwa katika muda uliowekwa kabla ya kukutana tena mwaka 2021 mjini Windhoek, Namibia. Tume itapitia utekelezaji wa makubaliano hayo kila baada ya robo mwaka,” amesema Nandi -Ndaitwa.