Tanzania kuonekana Bolywood

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jaji mstaafu Thomas Mihayo (kushoto) akiwa na mtayarishaji wa filamu wa Bollywood Raj Suri Harvinder na muongozaji Amandeep Singh. Wawili hao wapo nchini kwa ajili ya kuangalia maeneo ya kupigia picha za filamu zao watakapokuja kufanya kazi hiyo Oktoba mwaka huu.

Muktasari:

Mtayarishaji wa filamu za Bolywood atua bongo kuangalia maeneo ya kupigia picha za filamu


Wasanii wa filamu nchini wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujio wa wageni wanaokuja kufanya kazi za sanaa kujifunza na kuwa sehemu ya kutanganza utalii.

Hayo yameelezwa leo Septemba 10 na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji mstaafu Thomas Mihayo wakati akizungumza na waandishi juu ya ujio wa msanii wa filamu wa Bollywood, Raj Suri Harvinder Singh.

Singh ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya 3rd Rock Multimedia ya India yupo nchini kwa ajili ya kuangalia maeneo ya kupiga picha kwenye filamu zao.

Jaji Mihayo ameeleza kuwa ni fursa kubwa kwa mandhari na vivutio vya Tanzania kutumika kwenye filamu za Bollywood, hivyo nafasi hiyo inatakiwa kutumiwa vyema na wasanii wa Tanzania.

Amesema Singh na muongozaji wa video wa kampuni hiyo  Amandeep Singh wametangulia kuangalia ni vifaa vipi vitahitajika  kulingana na mazingira ya Tanzania.

Baada ya kufanikisha hilo Singh na wasanii 40 wanatarajiwa kuja nchini Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kazi ya upigaji picha hizo za filamu.

“Ni fursa nyingine tunaipata mwaka ni mafanikio kwetu kwa jinsi tulivyohangaika kuipata kampuni kubwa namna hii na wameonekana kuvutiwa na vivutio vyetu,”

“Hii itasaidia kuendelea kupenya kwenye soko la India maana kama mazingira yetu yataonekana kwenye filamu zao na wakiweka picha katika mitandao ya kijamii watatusaidia kutangaza,” amesema Jaji Mihayo

Kwa upande wake Singh amesema amefurahishwa na mazingira ya Tanzania na yanafaa kwenye kazi zake.

“Kwa ujumla mazingira yanavutia tutakuja wasanii 40 ni wengi na hao ni mchanganyiko wa filamu na muziki lengo ni kupata kitu tofauti na itasaidia kuonyesha Tanzania kuna nini,”

“Tunategemea kufanya kazi na wasani, wanamuziki na watayarishaji wa Tanzania ili kutusaidia tuweze kutengeneza vitu vizuri zaidi kulingana na uzoefu wao,”

Akizungumzia ujio huo muigizaji Issa Kipemba amesema ni fursa kwao kujifunza namna wenzao wa Bollywood wanavyoandaa filamu zao ambazo zina soko kubwa duniani.