Serikali ya Tanzania yafikiria likizo miezi sita wanaojifungua watoto njiti

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Balozi Augustine Mahiga

Muktasari:

Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Balozi Augustine Mahiga amesema ombi la wanawake wanaojifungua watoto njiti kupewa msaada wa chakula na likizo ya miezi sita kwa wafanyakazi linahitaji mchakato wa kisheria.

Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Balozi Augustine Mahiga amesema ombi la wanawake wanaojifungua watoto njiti kupewa msaada wa chakula na likizo ya miezi sita kwa wafanyakazi linahitaji mchakato wa kisheria.

Balozi Mahiga ameyasema hayo leo Ijumaa, Novemba 15, 2019 katika kongamano la wiki ya mtoto njiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dar es Salaam wakati akijibu hoja iliyotolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mama Getrude Mongela.

Awali, akizungumza katika kongamano hilo, Mongela amesema kwakuwa wanakaa kutunza watoto katika vifua vyao kwa kipindi kirefu, wanahitaji chakula kwani kinamama hao wanawalea wakiwa hospitalini hivyo wanakuwa hawana uwezo wakutafuta.

“Si hili pekee kwa wale wanaofanya kazi kuna haja ya kuongezwa siku za maternity kutoka miezi mitatu wanataka iwe miezi sita hili linawafanya wengi wanaacha kazi kwa ajili ya kulea watoto,” amesema Mama Mongela.

Balozi Mahiga amesema ombi hilo haliwezi kujibiwa kwa sasa kwani kuna mambo ya kisheria hivyo ni suala ambalo linahitaji mashauriano ya wadau mbalimbali ikiwemo wizara ya Afya, Tamisemi na Wizara zingine.

“Kama waziri wa sheria siwezi kusimama na kusema nimelipitisha, ni suala ambalo linahitaji mashauriano, tupo wadau wengi kikubwa ni kwamba tuelewe matatizo ambayo mmeyaeleza hapa nimeyaelewa nimeyachukua,” amesema.