Tawiri watakiwa kufanya utafiti wanyamapori kuvamia makazi ya watu

Wednesday December 4 2019

Waziri wa maliasili na Utalii Dk Hamis

Waziri wa maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangala akizungumza na waandishi habari baada ya kufungua mkutano wa Tawiri jijini Arusha Leo. Picha Mussa Juma 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini(Tawiri) kufanya utafiti utakaosaidia kupunguza migogoro kati ya wananchi na wanyamapori.

Dk Kigwangalla ametoa agizo hilo leo Jumatano Desemba 4, 2019 katika ufunguzi wa mkutano wa 12 wa wanasayansi kutoka nchi 16 duniani.

Amesema hivi karibuni matukio ya wanyamapori kuua watu, kula mifugo na kuharibu mazao yameongezeka.

“Hali hii inasababisha baadhi ya watu kuanza kuua wanyama,  tunataka mfanye tafiti  na kushauri namna bora ya kupunguza migogoro hii" amesema.

Amesema mamba wanakula watu katika mto Ruvuma na Ruvu, kwamba unatakiwa ufanyike utafiti kubaini njia bora za kuzuia matukio hayo.

Mkurugenzi mkuu wa Tawiri,  Dk Simon Mduma amesema tayari wamebaini ongezeko la migogoro hiyo na wameanza kuifanyia kazi, moja ya njia ya kuzuiwa ni kuweka uzio wa miti ili mamba wasifike katika makazi ya watu.

Advertisement

“Pia tunaendelea na utafiti kuhusu simba na tembo ili kudhibiti matukio ya watu kuuawa na mifugo na kupata uzoefu kutoka nchi nyingine kama India ambako kuna wanyama lakini hakuna matukio mengi ya aina hii,” amesema.

Advertisement