Tetemeko la ardhi lazua taharuki Katavi, watoto wawili wajeruhiwa

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera

Muktasari:

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 55 vipimo vya Ritcha limetokea mkoani Katavi nchini Tanzania na kusababisha madhara ya nyumba kutengeneza nyufa pamoja na kujeruhi watoto wawili.

Katavi. Hofu imetanda kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi nchini Tanzania kufuatia kuibuka tetemeko la ardhi ambalo linakadiriwa kuwa na ukubwa wa 5.5 katika vipimo vya Ritcha.

Akizungumza na Mwananchi  Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumatatu Septemba 9, 2019 saa 9:40 usiku.

Homera amesema watoto wawili wa familia ya Magashi Itenga mkazi wa kijiji cha Jilabela  Manispaa ya Mpanda,  wamejeruhiwa na kupata majeraha madogo baada ya  kuangukiwa na ukuta wa nyumba wakiwa wamelala .

“Tetemeko hili limedumu kwa dakika tatu, mpaka sasa tumepokea taarifa za  watoto wawili, miaka saba na mwingine minane, wameangukiwa na ukuta,  walipata matibabu katika zahanati ya Inteka na hali zao zinaendelea  vizuri,” amesema Homera.

Amesema hakuna madhara mengine yaliyojitokeza tofauti  na  hilo, licha ya nyumba nyingi kupata nyufa kutokana na kuta  kubomoka.

Kamishina wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  Mkoa wa Katavi,  Regina Kaombwe amewataka wananchi  kuchukua tahadhari ya kujikinga na maafa kupitia elimu wanayowapatia.

“Wananchi  watumie elimu tunayowafundisha walale uvunguni mwa kitanda na wasimame  kwenye nguzo za nyumba pindi wanapoona viashiria vya tetemeko la ardhi, wasitoke nje maana ni hatari,” amesema  Regina.

Amina Rajabu ni mkazi wa Majengo  Manispaa ya Mpanda amesema  tetemeko hilo halijawahi kutokea na limesababisha mshtuko mkubwa.

“Kwa kweli lilikuwa babu kubwa sijawahi kuliona, mimi nilitoka nje nikasahau watoto ndani, cha kushangaza limerudia kama mara tatu ila naamini mwaka huu kutakuwa na mvua ya kutosha,”amesema  Amina.

Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Katavi,  Benjamini Kuzaga amesema licha ya kutokea tetemeko hilo bado hawajapokea taarifa za madhara yoyote yaliyotokea.

“Limetokea ila Jeshi la polisi hatujapata taarifa za mtu kuripoti kupata madhara  yaliyosababishwa na tetemeko hilo,” amesema Kuzaga.