Trump amtimua waziri wa ulinzi

Donald Trump

Muktasari:

Mark Esper ni waziri wa nne wa ulinzi katika kipindi cha miaka minne ya Rais Donald Trump ambaye amnebakiza wiki kumi kukaa ikulu.

Donald Trump jana Jumatatu (Novemba 9) amemtimua Waziri wa Ulinzi Mark Esper, akionekana kuiyumbisha zaidi serikali ambayo inakabiliwa na hali ya sintofahamu kutokana na rais huyo kukataa kukubali kushindwa na Joe Biden wa Demoratic.

Zikiwa zimebaki wiki kumi kukaa ikulu ya White House, hatua hiyo imezidisha wasiwasi kuwa Trump anaweza kuwageukia maofisa wengine wa usalama wa taifa ambao ameeleza wazi kuwa haridhishwi na utendaji wao.

Kwa mujibu wa ripoti kadhaa, Trump anaaminika kuwa anafikiria kumtimua mkurugenzi wa shirika la kijasusi la FBI, Chris Wray na mkurugenzi wa shirika la intelijensia la CIA, Gina Haspel, akionekana kuchukizwa kwamba hawakumuunga mkono katika mapambano ya kutaka arejee madarakani.

Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa Trump alishamtimua ofisa aliyehusika na programu ambayo ilitayarisha ripoti ya serikali kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, hatua ambayo ingeruhusu nafasi yake ichukuliwe na mtu ambaye anakaribia kufanana na mtazamo wa Trump kuhusu kuongezeka kwa joto duniani.

Kutimuliwa kwa Esper kulisababisha wanasiasa maarufu na viongozi wa zamani waonye wakimtaka asiyumbishe zaidi serikali.

Seneta Mark Warner, kiongozi mwandamizi wa Democratic aliyemo katika kamati ya intelijensia ya seneti, alisema "amekasirishwa sana" na kuondolewa kwa Esper.

"Kitu cha mwisho ambacho nchi yetu inahitaji ni kuongezeka kwa msukosuko katika taasisi zilizoundwa kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa letu," alisema Warner katika taarifa yake.

"Rais Trump asiongeze msukosuko kwa kuondoa kiongozi yeyote wa usalama wa taifa aliyeidhinishwa na seneti katika muda wake uliosalia ofisini," alisema.

Esper ni waziri wa ulinzi wa nne kwa Trump katika kipindi cha miaka minne, na kuondolewa kwake kumethibitisha kutokuwepo kwa uhusiano mzuri kati ya makao makuu ya jeshi, Pentagon na rais.

Kama waliomtangulia, Esper, 56, aliamua kutojiweka machoni pa wanasiasa kuepuka hasira za Trump.

Lakini wawili hao waligongana wakati ikulu iliposhinikiza jeshi lipeleke vikosi kupambana na waandamanaji, na nia ya Trump kuondoa mara moja vikosi vya Marekani nchini Afghanistan kabla ya jeshi kuhakikisha kuwa kufanya hivyo ni salama.

"Mark Esper amefukuzwa," Trump aliandika katika akaunti yake ya Twitter janay.

"Ningependa kumshukuru kwa kazi yake."