Advertisement

Trump ashauri Misri ilipue bwawa Ethiopia

Saturday October 24 2020
trumpypic

Washington, Marekani (AFP). Rais wa Marekani, Donald Trump jana Ijumaa alieleza hasira yake kwa Ethiopia baada ya kujenga bwawa kubwa katika Mto Nile na akaonekana kupendekeza kuwa Misri iliharibu.

Trump alitoa maneno hayo wakati akitangaza makubaliano ya kutuliza hali kati ya nchi washirika wa Marekani, Israel na Sudan, ambayo kama Misri, inahofia Ethiopia itatumia vibaya rasilimali hiyo adimu.

"Ni hali ya hatari sana kwa sababu Misri haitaweza kuishi kwa njia hiyo," Trump aliwaambia waandishi wa habari katika ofisi yake huku viongozi wa Sudan na Israel wakiwa katika simu.

"Wataishia kulilipua bwawa. Na nilisema hilo na nalisema kwa sauti na kwa uwazi -- watalilipua hilo bwawa. Na wanatakiwa wafanye kitu," alisema Trump.

"(Ethiopia) Walitakiwa wafute mpango huo (wa kujenga bwawa) kabla hata hawajaanza ujenzi," alisema Trump, akisikitika kuwa Misri ilikuwa katika vurugu za ndani ya nchi wakati ujenzi wa bwawa hilo, maarufu kwa jina la Grand Ethiopian Renaissance Dam, ulipoanza mwaka 2011.

Trump -- rafiki wa karibu wa Abdel Fattah al-Sisi, jenerali wa jeshi aliyeshika urais -- alikubali ombi la Misri la kumtaka awe msuluhishi kuhusu bwawa hilo, huku waziri wa fedha, Steven Mnuchin akiongoza mazungumzo.

Advertisement

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema mwezi Septemba kuwa inafuta msaada kwa Ethiopia kutokana na mpango wa nchi hiyo kuanza kujaza maji bwawa hilo licha ya kutofikia makubaliano na nchi hiyo.

"Nilishakamilisha makubaliano nao na bahati mbaya  Ethiopia ikayakiuka, kitu ambacho hawakutakiwa kukifanya. Hilo lilikuwa kosa kubwa," alisema Trump.

Misri inategemea Mto Nile kwa asilimia 97 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kunywa.

 

Advertisement