Tundu Lissu aingia mkataba na kampuni ya kimataifa kulinda haki zake

Muktasari:

Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu ameingia mkataba na kampuni ya kimataifa ya huduma za sheria ya Amsterdam and Partners LLP kwa ajili ya kulinda haki zake za kikatiba na kimataifa.


Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu ameingia mkataba na kampuni ya kimataifa ya huduma za sheria ya Amsterdam and Partners LLP kwa ajili ya kulinda haki zake za kikatiba na kimataifa.

Katika taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jana Jumatano Oktoba 2, 2019 imesema katika makubaliano yao, watahakikisha wanasimamia kwenye masuala ya kisheria na mahakama za kimataifa.

Imesema lengo ni kuhakikisha haki za mwanasheria mkuu huyo wa Chadema zinajulikana.

Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma nchini Tanzania akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge leo Jumamosi ya Septemba 7, 2019 amefikisha miaka miwili akiwa ughaibuni.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma kisha usiku wa siku hiyo hiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi ambako bado yuko huko mpaka sasa.

“Tunajivunia kufanya kazi na Tundu Lissu kumsaidia kuongeza uelewa kwenye hali yake na kampeni za uvunjifu wa sheria za kuzuia  kuminywa kwa haki na uhuru wa vyama vya siasa,” amesema Robert Amsterdam ambaye ni mwanzilishi wa kampuni.

Kwa upande wake Lissu amesema makubaliano yao ni muhimu.

“Tunatazamia kufanya mambo mengi na Amsterdam kwa sababu ana uzoefu mkubwa wa masuala mbalimbali” amesema Lissu

Kampuni ya kimataifa ya huduma za sheria ya Amsterdam and Partners LLP imefanya kazi na watu mashughuli duniani wakiwemo mbunge wa Kyondo Mashariki na mwanamuziki Bobi Wine, Rais mstaafu wa Zambia,  Rupiah Banda na viongozi mbalimbali.