Tundu Lissu akamatwa na polisi

Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu.

Muktasari:

  • Makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ambaye alikuwa mgombea urais kupitia Chadema katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 amekamatwa na polisi leo jijini Dar es Salaam akiwa anatokea ofisi za umoja wa Ulaya.

Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Tundu Lissu amekamatwa na polisi jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Novemba 2, 2020 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema Lissu amekamatwa leo jioni akiwa anatokea ofisi za umoja wa Ulaya zilizopo Dar es Salaam nchini Tanzania.

“Ni kweli Lissu tumemkamata, alikuwa anatokea ofisi za umoja wa ulaya na hivi tunavyozungumza ndio tunaingia naye kituoni. Ila ukweli ni kwamba tumemkamata.” amesema Mambosasa.

Kamanda huyo amesema Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema anatuhumiwa kupanga kufanya maandamano bila kufuata utaratibu.

Usiku wa kuamkia leo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; mwenyekiti wa Chadema kanda ya Kaskazini, Godbless Lema pamoja na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Boniface Jacob walikamatwa na polisi wakiwa kwenye kikao.

Mbali na viongozi hao, zaidi ya wanachama 30 wa chama hicho maeneo mbalimbali nchini wamekamatwa na polisi leo wakidaiwa kutaka kushiriki maandamano.