Uchaguzi naibu Meya Iringa waahirishwa, kura ya siri yatajwa kuwa sababu

Mkurugenzi wa manispaa ya Iringa Hamid Njovu kulia akiahirisha baraza la madiwani la manispaa ya Iringa baada ya kutokea sintofahamu ya ukiukwaji wa kura ya siri wakati wa uchaguzi wa Naibu Meya.

Muktasari:

  • Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Iringa,  Hamid Njovu ameahirisha baraza la madiwani la Manispaa hiyo kufanya uchaguzi wa naibu Meya kutokana na kuibuka sintofahamu ya tafsiri ya kura ya siri.

Iringa. Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Iringa,  Hamid Njovu ameahirisha baraza la madiwani la Manispaa hiyo kufanya uchaguzi wa naibu Meya kutokana na kuibuka sintofahamu ya tafsiri ya kura ya siri.

Amechukua uamuzi huo kutokana na kuibuka mkanganyiko wa madiwani wa CCM na Chadema walioshindwa kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi

Akiahirisha uchaguzi huo leo Jumatano Oktoba 16, 2019, Njovu amesema hawawezi kufanya uchaguzi leo kwa sababu madiwani wamezua mjadala kuhusu sheria za upigaji kura, kuwataka wakapitie sheria na uchaguzi utafanyika wakati mwingine.

“Naahirisha baraza hili mpaka wakati mwingine nawaomba wajumbe mkasome sheria na kanuni za uchaguzi ili kukwepa kukiuka masharti ya kupiga kura,” amesema Njovu.

Diwani wa Mwangata (CCM), Nguvu Chengula ameunga mkono kuahirishwa kwa baraza hilo kwa sababu madiwani wanaokinzana na utaratibu wa kisheria wa upigaji kura wanakwenda kinyume na sheria.

 “Mjadala umeanza baada ya kuambiwa nini kinatakiwa kuonekana katika karatasi ya kupigia kura, kisheria kinachotakiwa kuonekana ni alama ya vema peke yake,” amesema.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amesema Chadema hawajapendekeza kanuni mpya kama CCM wanavyodai na walikuwa tayari kupiga kura lakini badala yake CCM walianza kujadili kura ambazo hazijapigwa.

“Kanuni ziko wazi kama kura zitakuwa zimeharibika zitahesabiwa kuwa si kura halali, tulichokuwa tunataka sisi wasituwekee masharti na kutupangia ni namna gani ya mtu apige kura,” amesema Mchungaji Msigwa.

Amesema ilitakiwa kusubiri kura zipigwe na ambazo si halali kuhesabiwa,  kwa mujibu wa kanuni ziondolewe na mshindi aweze kutangazwa.

Amesema katika uchaguzi huo Chadema walikuwa na mikakati yao na lengo lilikuwa kumkamata msaliti  hata kama kura ingeharibika.

“Tulikubaliana madiwani wote pamoja na wabunge wawili waweke alama itakayomuonyesha amepiga kura kama haweki tumjue msaliti wetu,” amesema Mchungaji Msigwa.