Uchunguzi ajali iliyoua wafanyakazi watano TRC kufanyika kwa siku saba

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amemuagiza mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa kuunda timu ya uchunguzi wa ajali ya treni iliyosababisha vifo vya wafanyakazi watano wa shirika hilo.

Korogwe. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amemuagiza mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa kuunda timu ya uchunguzi wa ajali ya treni iliyosababisha vifo vya wafanyakazi watano wa shirika hilo.

Amesema timu hiyo itaongozwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) itawasilisha taarifa katika wizara hiyo ndani ya siku saba kuanzia leo Jumanne Machi 24, 2020.

Ametoa agizo hilo jana jioni Jumatatu Machi 23, 2020 alipotembelea eneo ilipotokea ajali hiyo. naibu waziri huyo pia alitembelea hospitali ilikohifadhiwa miili hiyo.

Ajali hiyo ilihusisha treni ya uokoaji iliyogongana na kiberenge kati ya stesheni za Mwakinyumbi na Gendagenda katika reli ya Dar-Kilimanjaro na kusababisha vifo vya watumishi hao, wakiwamo mameneja watatu.

Kwa mujibu wa Jamila Mabrouk ambaye ni mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa TRC, wanne walifariki papo hapo wakati wawili walipelekwa hospitali na mmoja akafariki dunia baadaye.

 Waliofariki katika ajali hiyo ni Ramadhani Gumbo, ambaye ni meneja usafirish-aji Kanda ya Tanga, Fabiola Mushi (meneja ukarabati wa mabehewa ya abiria wa Kanda ya Dar es Salaam) na Joseph Komba (meneja msaidizi wa usafirishaji Kanda ya Dar es Salaam).Wengine ni mtaalamu wa usalama wa reli, Philbert Kajuna na dereva wa kibe-renge, George Urio.

Nditiye amesema uchunguzi unafanyika kwa kuwa tukio hilo aliloliita kuwa si la kawaida limeisababishia Serikali hasara kwa kupoteza wataalamu wake.

“Mabehewa  kujiendesha yenyewe na kugongana na kiberenge siyo kitu cha kawaida sana, imetuuma  sana Serikali kupoteza wataalamu hawa,” amesema Nditiye.

Naye Kadogosa aliwahakikishia wateja wa shehena  ya saruji iliyokuwa katika mabehewa yaliyoanguka kufikishwa katika maeneo husika.

“Niwahakikishie wateja wetu shehena ya saruji iliyokuwa  itafikishwa mapema kwa sababu timu ya wataalamu ipo eneo la tukio kwa ajili ya marekebisho ya mwishom,” amesema  Kadogosa.