Uchunguzi kujipiga risasi mwanafunzi Arusha unaendelea

Muktasari:

Polisi Mkoa wa Arusha nchini Tanzania inaendelea na uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 19 anayedaiwa kujiua kwa kujipiga risasi kwa silaha ya baba yake.

 


Arusha. Uchunguzi wa tukio la kujiua kwa mwanafunzi Faisal Salim (19)  wa shule ya Sekondari Arusha Meru nchini Tanzania aliyejipiga risasi kwa kutumia  bunduki ya baba yake jana Jumapili alfajiri ya saa 11 Agosti 18,2019 unaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amesema bado uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hakuna mtu aliyekamatwa.

Katika nyumba aliyokuwa anaishi mtoto huyo na baba yake, Salimu Ibrahimu leo Jumatatu Agosti 19,2019  imefungwa na mmoja wa majirani zake akidai msiba  wa mwanafunzi huyo umehamishwa kwa mama yake.

Juma Rashid ambayue ni jirani alisema mwanafunzi huyo amezikwa jana Jumapili katika makaburi ya Njiro jijini Arusha nchini Tanzania.

"Huyu mtoto alikuwa anaishi na baba yake tu, baada ya baba yake katengana na mama yake" amesema Rashid

Jitihada za kumpata baba mzazi wa mwanafunzi huyo bado zinaendelea.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi