OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Uganda yaishtaki Israel Umoja wa Mataifa-13

Muktasari:

Katika toleo lililopita tuliona jinsi mwandishi wa Israel, Uri Dan alivyokuwa akimhoji Rais wa Uganda, Idi Amin, kwa njia ya simu kutoka Tel Aviv, Israel. Katika mahojiano hayo Amin alikanusha akidai kuwa jeshi lake halikushirikiana na watekaji nyara. Alisema wanajeshi hao walikuwako uwanjani kulinda maisha ya Waisraeli.

Katika toleo lililopita tuliona jinsi mwandishi wa Israel, Uri Dan alivyokuwa akimhoji Rais wa Uganda, Idi Amin, kwa njia ya simu kutoka Tel Aviv, Israel. Katika mahojiano hayo Amin alikanusha akidai kuwa jeshi lake halikushirikiana na watekaji nyara. Alisema wanajeshi hao walikuwako uwanjani kulinda maisha ya Waisraeli.

Wakati akiendelea kuhojiwa na mwandishi Uri Dan wa Israel, Idi Amin alisema nia yake ilikuwa ni kuokoa maisha ya mateka wa Kiyahudi ambao walikuwa wanashikiliwa na magaidi katika uwanja wa ndege wa Entebbe. Sehemu ya mwisho ya mahojiano hayo ilikuwa hivi:

Dan: Je, unakusudia kutangaza hali ya hatari?

Idi Amin: (Alinyamaza)

Dan: Je! Hauogopi kwamba, baada ya operesheni kama hii, na baada ya pigo kama hilo, unaweza kupoteza urais wa Uganda?

Idi Amin: (Baada ya kusita kidogo kujibu) Hapana, hapana! Kwa kweli sivyo! Wanajeshi wangu wako pamoja nami, na wananisaidia, na hakuna shida hata kidogo.

Dan: (Anarudia swali) Je, utatangaza hali ya hatari?

Idi Amin: Ndiyo.

Kwa hilo swali la kutangaza hali ya hatari au la, dakika chache baadaye alitafakari na kisha akajibu “Kwanini nitangaze?”

Dan: Kwa hiyo serikali yako itamudu na kudumu?

Idi Amin: Hapana. Serikali yangu iko salama kabisa. Na jambo lililotokea ni dogo sana. Mtaona.

Dan: Swali la mwisho Mheshimiwa Rais. Utashtaki hili jambo kwa Umoja wa Mataifa au, angalau, kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU)?

Idi Amin: Siwezi kuzungumza hayo kwenye simu. Kwaheri!

Ingawa Idi Amin alisema wanajeshi wake hawakutaka kupigana, aliyekuwa Waziri wa Afya wa Uganda, Henry Kyemba katika kitabu chake, ‘State of Blood: The Inside Story of Idi Amin’, aliandika hivi:

“Idi Amin, kama ilivyokuja kubainika baadaye, aliposikia mashambulizi (ya ndege za Israel) alidhani ni maasi ya kijeshi kutoka taifa la nje Kenya, labda au Tanzania. Hakuweza kung’amua ukweli kwa sababu mara tu mashambulizi yalipoanza maofisa waandamizi wa jeshi lake walikimbia kujificha.

“Wakati mashambulizi yamepamba moto ilikuwa ni saa 5:45 usiku, maofisa waandamizi waliohusika na uwanja wa ndege (wa Entebbe) walikuwa wakinywa na kucheza dansi ‘Lake Victoria Hotel’ karibu na Ikulu. Wakati makomando wa Israel walipotua, na waliposikia mlipuko wa kwanza uliwafanya watimke na kwenda kujificha, wakiwaambia watu wa familia zao kama watapigiwa simu waseme hawapo. Hadi ilipojulikana nani anapigana na nani, hakuna ofisa yeyote aliyetaka kushiriki upande wowote. Idi Amin pia alikimbia kujificha katika chumba cha madereva cha jengo la Ikulu.”

Baada ya mateka kukombolewa mjini Entebbe na kufikishwa Israel kupitia Kenya, Serikali ya Uganda ililipeleka suala hilo Umoja wa Mataifa. Kazi hiyo ilifanywa na ujumbe wa Uganda ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Kanali Juma Oris Abdallah.

Siku tano baada ya shambulio la Israel, Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ulipeleka malalamiko yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu “kitendo cha uchokozi” kilichofanywa na Israel dhidi ya Uganda.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Kanali Juma Oris Abdallah na mwakilishi wa Mauritania, Moulaye El Hassen walizungumza kwa niaba ya kundi la Afrika, wakisema kuwa uvamizi wa Israel nchini Uganda umekiuka kifungu cha 2(4) cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa kuvamia uhuru wa ndani wa nchi mwanachama wa umoja huo.

Katika mkutano huo Kanali Abdullah alisema Uganda inapenda kutoa shukrani zake kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika kwa kuomba kuitishwa kwa mkutano wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafakari uchokozi wa Israel dhidi ya nchi huru ya Uganda yenye heshima kimataifa. Ujumbe wangu unapenda pia kulishukuru Baraza la Usalama kwa kukubali kuitisha mkutano huu.

Kisha akaendelea, “Majira ya saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, Juni 28, 1976, Mheshimiwa Al-Hajji Field-Marshal Dk. Idi Amin Dada, V.C., D.S.O., M.C., Rais wa Maisha wa Jamhuri ya Uganda, aliarifiwa kwa simu kutoka Uwanja wa Ndege wa Entebbe kwamba ndege ya Ufaransa ilikuwa imetekwa ikiwa na watu 250 na ilikuwa ikizunguka anga la Entebbe, ikiwa imebakiza mafuta ya kutumika kwa dakika 15, na ilikuwa ikiomba ruhusa ya kutua.”

Kanali Abdullah alisema baada ya Rais Amin kupata taarifa hizo akajikuta yuko katika kigugumizi cha ama kuikatalia ndege kutua lakini ianguke na kuua abiria wote wa ndege hiyo na wafanyakazi wake au airuhusu itue lakini akabiliane na matokeo ya utekaji huo.

Alisema baada ya Idi Amin kuyatafakari yote hayo, na kwa kuzingatia hali ya kiutu, aliamuru ndege hiyo iruhusiwe kutua salama katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe. Kikosi cha wanajeshi kilipelekwa uwanjani hapo kukabiliana na hali yoyote ya hatari ambayo ingeweza kutokea.

Nchi kadhaa zililaani kitendo cha Israel kuivamia Uganda, lakini balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Chaim Herzog alipinga vikali maelezo ya Uganda na akatoa kile alichosema ni ushahidi wa Uganda kushirikiana na watekaji nyara na hivyo kuwa wa kwanza kuvunja sheria za kimataifa kwa kushirikiana na magaidi.

Chaim aliirushia sana lawama serikali ya Uganda na wote wale waliokuwa wanaitetea. Alisema anasimama mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa . “Nasimama hapa kama mlalamikaji anayelilalamikia shirika hili, Umoja wa Mataifa, ambao kwa sababu ya kuwa na wawakilishi wengi Waarabu na wafuasi wao umeshindwa kuchukua hatua madhubuti ili kupambana na ugaidi na uovu unaosababishwa na ugaidi duniani.”

Kwa mujibu wa kitabu ‘Outlaw Territories: Environments of Insecurity/Architectures of ...’ cha Felicity D. Scott (uk. 423) Hassen (mwakilishi wa Mauritania) alihoji kuwa ikiwa ndege ya Ufaransa iliyotekwa isingepelekwa Uganda lakini ikapelekwa kwingine kama Marekani, Ufaransa, Ubelgiji au Uingereza, “nchi hizo zingenyamaza kimya ikiwa zingeshambuliwa kama Uganda si tu kwa kuingiliwa mamlaka yake bali pia na raia kuuawa na wanajeshi kuuawa? Haingekuwa hivyo, na wala Israel wasingefikiria hata uvamizi huo. Lakini kwa kuwa iliyotendwa ni nchi ya dunia ya tatu, nchi ya Kiafrika, ndiyo maana inapuuzwa.”

Marekani ilitetea uhalali wa Israel kuvamia na kuishambulia Uganda, lakini iliunga mkono kwa uangalifu sana. Katika Umoja wa Mataifa, Balozi William Scranton alisema tukio la Israel kuivamia Uganda ni halali kwa sababu lilikuwa ni “hali ya kipekee”.

Baada ya mjadala wa siku nne, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikuchukua hatua zozote dhidi ya Israel. ‘The United Nations and the Control of International Violence: A Legal and Analysis’ cha John Francis Murphy kinaandika: “Julai 14 (1976) Marekani na Uingereza wakapitisha azimio la kuifanya Baraza la Usalama kulaani utekaji nyara na vitendo vyote vinavyotishia maisha ya abiria na wafanyakazi wa ndege na usalama wa anga wa kimataifa. Mwishowe Israel waliibuka tena kama washindi.

Itaendelea kesho…