Uhaba wa samaki waikabili Tanzania

Muktasari:

Licha ya kupungua kwa samaki, Tanzania  ina ukanda wa uchumi wa bahari wenye ukubwa wa kilometa za mraba 223,000 ambazo hazijawekezwa.

Dar es Salaam. Tanzania inakabiliwa na uhaba wa tani zaidi ya 300,000 za samaki kwa mwaka kutokana na kutokukua kwa sekta ya uvuvi kulingana na ongezeko la idadi ya watu.

Akizungumza leo Ijumaa Septemba 13, 2019 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid Tamatamah amesema tangu miaka ya 1990 uvuvi umekuwa kati ya tani 350,000 hadi 400,000 kwa mwaka.

"Katika kipindi hicho idadi ya watu imeongezeka kutoka watu 25 milioni hadi 55 milioni. Hali hii imesababisha kushuka kwa kiasi cha samaki kiliwacho kwa kila mtu kwa mwaka kutoka kilo 14 mwaka 1990 hadi kilo nane mwaka 2019," amesema Dk Tamatamah.

Amesema hali hiyo inatishia ustawi wa Taifa kwa kuwa samaki huchangia asilimia 1.7 ya pato la Taifa, huku ikiajiri zaidi ya watu 4 milioni.

Hata hivyo, amesema katika kipindi cha mwaka 2018/19 jumla ya tani 448,468 za samaki zimevuliwa zikiwa na thamani ya Sh2.11 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 15.72, kutokana na kudhibitiwa kwa uvuvi haramu.

"Vilevile mwaka 2018/19 jumla tani 51,718 za mazao ya uvuvi na samaki wa mapambo 81,373 wenye thamani ya Sh691.88 waliuzwa nje ya nchi," amesema Dk Tamatamah.

Ili kuongeza uzalishaji wa samaki, Dk Tamatamah amesema Serikali ina mpango wa kulifufua lililokuwa shirika la uvuvi (Tafico) ili kuwekeza kwenye ukanda wa uchumi wa bahari.