Uingereza yazungumzia uhusiano wake na Tanzania

Friday July 12 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Saalam. Serikali ya Uingereza imeihakikishia Tanzania kuendeleza ushirika katika masuala mbalimbali ya ubia wa maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wawekezaji kutoka Uingereza kuwekeza nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa masuala ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza Idara ya Ushirikiano wa Maendeleo, Harriett Baldwin alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa  Palamagamba  Kabudi, jijini London, Uingereza.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje nchini Tanzania leo Ijumaa Julai 12, 2019 inaeleza kuwa wawili hao wamezungumzia ushirikiano wa ubia wa maendeleo uliopo na kuonyesha kuridhishwa na Serikali ya Tanzania inavyosimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Uingereza.

Miradi hiyo ni iliyopo katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo na miundombinu ya barabara za vijijini sambamba na maboresho ya mifumo ya fedha, utumishi wa umma na Serikali za mitaa.

Baldwin ameipongeza Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa,  kuongeza ufanisi kwenye utoaji wa huduma katika sekta ya umma, kuongeza uwajibikaji na utawala bora.

Waziri huyo wa Uingereza ameyataja mambo hayo kama hatua muhimu ya kufikia malengo ya haraka na kuondoa umasikini.

Advertisement

Kwa upande Profesa Kabudi ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuwa mbia wa maendeleo na kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uwekezaji, biashara na utalii nchini Tanzania.

Advertisement