Ujenzi wa daraja lililokatika Moro-Dodoma waanza

Morogoro. Kazi ya matengenezo ya daraja lililokatika kati ya Dodoma-Dar es Salaam imeanza tangu usiku kwa kuweka vifusi na mawe huku madaraja mawili ya chuma yakiwa yanaunganishwa ili kufungwa kwenye eneo lilipokatika wilayani Kilosa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kuandikwa amesema hayo leo Jumanne Machi 3, 2020 katika eneo la tukio ambapo amesema tayari juhudi mbalimbali zimeanza na ujenzi wa madaraja mawili ya chuma yanatengenezwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inafanya matengenezo kwa haraka ili mawasiliano yaweze kuendelea kwani barabara hiyo inategemewa kiuchumi si kwa mikoa ya Kanda ya Kati na ziwa pekee bali hata nchi jirani za maziwa zikiwemo Uganda, Burundi, Congo.
Amesema muda si mrefu madaraja yatafungwa eneo hilo ili kupitisha maji na baadaye waanze kuweka mawe ya kutosha ili mawasiliano yarejee.
Amawataka wanaitumia barabara ya Morogoro-Dodoma kutumia njia mbadala hasa kwa magari madogo kupitia Morogoro –Iringa-Dodoma kwa pande zote mbili.

“Wataalamu wako eneo la tukio na wakati daraja lina katika mkurugenzi wa barabara nchini alikuwepo eneo la tukio kwa ajili ya ukaguzi na Serikali imejipanga katika kipindi hiki cha mvua wametawanyika nchini kote kwa ajili ya kukagua barabara hasa zile kuu zilizotengenezwa miaka mingi,”amesema.
Amesema mkurugenzi wa barabara alipofanya ukaguzi aligundua kuwepo kwa nyufa ambao ungeleta athari na kuanza kutoa taadhari jambo ambalo limesaidia kutokutokea maafa.
“Linapotokea tatizo tunaunganisha nguvu zote kwa maana ya Tanroad, wizara na taasisi nyingine wakiwemo wanaotengeneza SGR ambao wana vifaa vya kisasa, wataalam wa jeshi na hii inasaidia kutokana na mchanganyiko kwa kuunganishwa nguvu ya pamoja,” amesema.
Amesema lengo ni kuhakikisha ujenzi unakamilika na huduma zinarejea.
Waziri Kwandikwa amesema kwa utaratibu wa kawaida barabara inaishi hivyo barabara ya Morogoro-Dodoma umefika wakati wa kujengwa upya kwani ina zaidi ya miaka 30 tangu kujengwa kwake.