VIDEO: Ukweli kuhusu corona

Muktasari:

Ifahamike kuwa si kila anayeugua ugonjwa COVID -19 hufariki duniani. Virusi vinavyosababisha ugonjwa huu vimeuzua taharuki baada ya kusambaa kwa kasi duniani. Tangu juzi vimewapata wagonjwa watatu nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Ifahamike kuwa si kila anayeugua ugonjwa COVID -19 hufariki duniani. Virusi vinavyosababisha ugonjwa huu vimeuzua taharuki baada ya kusambaa kwa kasi duniani. Tangu juzi vimewapata wagonjwa watatu nchini Tanzania.

Virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19 vimesambaa katika nchi zaidi ya 100 duniani huku watu 179,111 wakiwa wameambukizwa na 11,525 wamepoteza maisha, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duania (WHO).

Hali hiyo imesababisha hali ya wasiwasi duniani, kutokana na kuenea kwake kwa haraka katika kipindi cha muda mfupi.

Hata hivyo, watu wanapaswa kuondoa hofu kutokana na ukweli kwamba takwimu zinaonyesha kwamba watu wengi wanapona baada ya kuugua ugonjwa huu. Pia mafanikio yamejidhihirisha kuwa pale masharti ya kujikinga yanapozingatiwa, basi kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza kasi ya maambukizi yake.

Kufikia jana, takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 79,000 duniani waliougua ugonjwa wa COVID-19 walikuwa mepona. Idadi ya wagonjwa 111 kati ya 179, walithibitishwa kupona baada ya uchunguzi wa WHO.

Watalaamu wanaeleza kuwa watu wengi walioumwa ugonjwa huu wamepona ingawa kuna idadi kubwa ya watu ambao pia hawakupona. Jambo muhimu la kuzingatia ni kwamba watu wanatakiwa kuzingatia masharti ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huu.

Rika linaloathirika

Watalaamu wa WHO bado wanafanya utafiti wa rika linaloathirika na virusi vya corona. Hata hivyo, takwimu kwa sasa zinaonyesha kuwa watu wazima hasa wenye umri mkubwa, ndio wameonekana kuathirika zaidi. Watu hao ni wale ambao pia wanaumwa magonjwa yanayopunguza kinga za mwili kama shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo, mapafu, saratani na kisukari.

Namna ya kujikinga

Nchini Tanzania watu wanaonekana kuwa na shauku ya kujua namna ya kujikinga dhidi yake.

Wengi wameonekana mitaani wakiwa wamevaa kinga za kuziba midomo na pua na wengine wamekwenda mbali zaidi kwa kujifunga vitambaa usoni ili kujikinga pua na midomo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Udhibiti Utafiliaji wa Magonjwa ya Milipuko, Dk Janeth Mghamba akizungumza jijini Arusha jana, aliwataka watumiaji wa vifaa vya kuziba mdomo na pua (maski), kuzingatia matumizi sahihi ili visiwaletee madhara badala ya kinga.

“Hizi ‘maski’ hazipaswi kutumiwa bila kuzingatia kanuni za kiafya. Zinatakiwa kutumiwa kwa saa nne kisha kubadilishwa, vinginevyo mtumiaji anaweza kujiweka katika mazingira hatarishi ya maambukizi ya magonjwa mengine,” alisema Dk Mghamba na kuongeza: “Na si kila mtu anatakiwa kuivaa bali watoa huduma, wenye maambukizi na kwenye mikusanyiko.”

Kadhalika kwa mujibu wa maelekezo ya Kituo cha Kinga na Kudhibiti cha Magonjwa (CDC) cha Chuo Kikuu cha California nchini Marekani, watuwapaswa kufahamu kuwa mtu halazimiki kuvaa kitu cha kujikinga pua na mdomo kama hana maradhi ya COVID-19.

“Tunafahamu kuwa kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya kujikinga mdomo na pua, lakini watu wanapaswa kuelewa vitu hivi vinahitajika zaidi kwa watu wanaoumwa,’’ inashauri CDC.

Tayari kuna ripoti nchini Tanzania kwamba kuna mahitaji makubwa ya vimiminika vya kinga tangu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutangaza kuwepo kwa mgonjwa wa COVID-19, Jumatatu iliyopita na jana wawili wameongezeka.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema watu wanapaswa kutochanganyiwa na upungufu za vimiminika vya kinga za magonjwa wakati huu wakijaribu kupambana kujikinga na virusi vya corona.

“Kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka ni bora zaidi kuliko kutumia vimiminika vya kinga. Usibabaike pale unapokosa vimimiminika vya kinga,” alisema Dk Ndugulile kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Twitter.

Maelezo ya Dk Ndugulile yanafanana na taarifa iliyotolewa mtalaamu wa masuala ya kinga na kudhibiti magonjwa wa WHO nchini Tanzania, Dk Grace Saguti, ambaye alisema kuwa virusi vya COVID-19 ni habari mpya na huchukua muda mrefu kuzaliana. “Kutokana na hali hiyo, kumekuwa na changamoto kubwa katika kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huu,” aliongeza Dk Saguti.