Prime
NIKWAMBIE MAMA: Mwanasiasa ndiye kiongozi
Muktasari:
- Mwanasiasa makini hufanya siasa katika muda wake wote maishani. Anaweza kupangilia vipindi na matukio bila kuathiri maisha ya watu wengine. Atasikiliza shida za watu wake, atapanga na kutekeleza malengo, atasimamia utekelezaji wa sera na kadhalika.
Siasa ni mchakato wa kuongoza, kusimamia, na kufanya maamuzi kuhusu mambo ya jamii au taifa. Inahusisha jinsi mamlaka yanavyopatikana na kutumiwa ili kutekeleza sheria, sera, na mipango ya maendeleo.
Kwa vile siasa inashughulikia watu, imekuwa sehemu ya maisha ya mwanadamu. Kwenye maisha ya sasa, hakuna jamii inayoweza kujitenga na taratibu za kilimwengu. Na ingelikuwapo ni lazima ingeulizwa.
Siasa ni kama pumzi ya mtu, haikwepeki. Ni sawa na basi au ndege inayosafirisha abiria, meli au lori inayopeleka mizigo, n.k. Pengine ni sawa na droni inayobeba mabomu.
Ili abiria na mzigo uweze kusafiri ni lazima upakie kwenye chombo. Na chombo hakiwezi kwenda bila kuendeshwa.
Vijana wa leo watanipinga kwa hoja kuwa droni hazihitaji dereva, lakini nawaambia kuwa hata mrusha nyungo ni dereva.
Siasa ndio chombo kinachosafirisha watu, bidhaa, huduma na kadhalika. Mkiwa na mwanasiasa mzuri mtasafiri bila misukosuko hata kama mtapita kwenye dhoruba na tufani.
Wakati mwingine mkiwa vitani dhidi ya maadui wa ndani (umasikini, ujinga na maradhi), mnashtukia bei ya mafuta ikipandishwa na vita ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Hapa ndipo nahodha mkwepa mawimbi anapoonesha umahiri wake.
Namwongelea zaidi mwanasiasa kuliko kiongozi kwa kuwa tofauti yao hapa nchini ni ndogo sana. Ni lazima mtu awe mwanachama wa chama cha siasa ili agombee nafasi ya uongozi wa umma.
Hivyo ni wazi kuwa siasa ndiyo inayoongoza nchi. Kama ndio hivyo, dereva wa siasa ni mwanasiasa. Huyu ndiye nahodha wa safari yetu.
Mwanasiasa makini hufanya siasa katika muda wake wote maishani. Anaweza kupangilia vipindi na matukio bila kuathiri maisha ya watu wengine. Atasikiliza shida za watu wake, atapanga na kutekeleza malengo, atasimamia utekelezaji wa sera na kadhalika.
Lakini wakati akiyafanya hayo, hutasikia migomo wakati akishughulika na kero na mapungufu yanayojitokeza wakati wote.
Nimesema kuwa mwanasiasa makini huifanya siasa kuwa sehemu ya maisha yake. Lakini wapo wanasiasa uchwara wanaowaza ukubwa tu. Hawa wataonekana na kusikika wakati wa uchaguzi tu, na wakati wa shida zingine hawafikiki.
Katika mataifa yote yanayoendelea, shida huwa ni sehemu ya safari yake. Haina tofauti na makuzi ya mtoto, ambapo homa zinakuwa sehemu ya makuzi.
Watu na maendeleo yao, wanachukua taswira ya mama anayesafiri nyikani akiwa na mwanaye. Lengo lao ni kufika kule wanakokwenda, na hakuna mmoja atakayependa kuwa mbali na mwenzake. Aliyetangulia angependa asimwache anayemfuata. Ndivyo ambavyo wananchi hawataki kuachwa na maendeleo. Kwa kifupi maendeleo kiuchumi yanatafsiriwa sambamba na maendeleo ya watu.
Ndio maana tunasema nchi yenye miundombinu ya kisasa na watu masikini bado haikidhi dhana ya maendeleo.
Tatizo la watu si maghorofa au magari kujazana nchini mwao, ila ni hali bora za wananchi. Nikisema hali bora namaanisha hali ya kuzimudu gharama za maisha.
Kama wanaziona shule na hospitali za kisasa, halafu wanashindwa kusomesha na kutibiwa kwa sababu ya gharama, bado wanakuwa chini kiuchumi.
Kwa vyovyote hawatakosekana watakaozimudu gharama kubwa. Lakini hiyo haimaanishi kuwa wananchi wanajiweza.
Wastani wao ni mdogo sana ukilinganisha na wenzao wasiojiweza kiuchumi. Ni vizuri tunakubaliana kuwa lengo la Serikali ni kumfanya kila mmoja aweze kuubeba mzigo wake.
Hapa ndipo tunapohitaji wanasiasa makini wanaoweza kusuka mipango na kutufikisha kwenye nchi ya ahadi.
Matatizo ya wengi yanafanana. Ni kero zilezile zinazojirudia bila kuisha. Kwa mfano wanapokubali kulipa kodi kwa ajili ya ulinzi wake na mali zao, halafu wakalazimika kulipia gharama za kusaka wahalifu wao.
Au mtu anapolazimika kulipia kipimo kilekile kila anapohamishiwa kwenye hospitali za juu. Ni mzigo mzito sana kwenye hospitali za umma; kujisajili hela, kumwona daktari hela, kupimwa hela, kupata dawa hela...
Ingelikuwa faraja kama wananchi wangepatiwa bima za afya bure. Hii ingepunguza mzigo wa gharama za matibabu na kuwapa uhakika wa kupata huduma wanapozihitaji.
Mwananchi anayefanya kazi kwa bidii anahitaji kuona kodi zake zikirejea kwake kwa namna ya huduma bora.
Asijisikie kuwa jukumu la Serikali linaishia kukusanya mapato pekee, bali pia kuhakikisha maisha yake yanakuwa nafuu na yenye matumaini.
Hapa ndipo siasa bora zinapotofautiana na siasa tantalila. Siasa bora huonekana kwenye matokeo yanayogusa maisha ya watu wa kawaida. Huonekana pale mkulima anapopata soko la mazao yake, mfanyabiashara anapopata mazingira mazuri ya kufanya biashara, na kijana anapopata fursa ya ajira au mtaji wa kuanzisha shughuli zake.
Wananchi hawajengi maisha yao kwa ahadi. Wanahitaji kuona mabadiliko halisi katika kipato, huduma na ustawi wao.
Mwisho wa yote, wananchi wanahitaji siasa zinazowajumuisha, siasa zinazowasikiliza na siasa zinazowatumikia. Nchi haiwezi kujengwa na Serikali peke yake wala na wananchi peke yao. Inahitaji ushirikiano wa pande zote mbili. Pale ambapo viongozi wanatimiza wajibu wao na wananchi wanatimiza wajibu wao, taifa husonga mbele kwa kasi zaidi.
Ndipo siasa zinapokuwa chombo cha maendeleo badala ya kuwa chanzo cha malalamiko, na ndipo safari ya kuelekea nchi ya ahadi inapopata mwelekeo wa uhakika.