VIDEO: Ulinzi waimarishwa tamasha la Jamafest Dar

Muktasari:

Tamasha la nne la utamaduni la Afrika Mashariki (Jamafest) linazinduliwa leo Jumapili, Dar es Salaam Tanzania na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan huku ulinzi ukiwa umeimarishwa na vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama nchini humo.

Dar es Salaam. Ulinzi umeimarishwa katika tamasha la nne la utamaduni la Afrika Mashariki (Jamafest) linalofanyika Uwanja vya Uhuru na Taifa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Tamasha hilo linazinduliwa leo Jumapili Septemba 22, 2019 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Tayari watu wameanza kuingia katika viwanja hivyo kwa kukaguliwa na mashine maalum huku vikosi mbalimbali ikiwamo polisi na Skauti vikiimarisha katika maeneo mengine.

Robert Kanga ambaye ni raia kutoka Kenya amesema ulinzi ni suala zuri kwa kuwa sehemu hiyo inakutanisha watu wengi na kila mtu ana akili zake.

"Hapa ni sehemu ambayo wanaingia watu mbalimbali na kila mtu ana akili zake, hivyo kukaguliwa ni jambo muhimu kwani wengine wanaweza kuingia na silaha zinazoweza kuwadhuru watu,” amesema Kanga

Mwajuma Sabri kutoka Mbagala Dar es Salaam amesema ukaguzi unaofanywa ni mzuri japokuwa wananchi wengine wana hofu kwa kuwa hawajui kama kuna kiingilio au ni bure.

Tamasha hilo linalozinduliwa leo litamalizika Septemba 28, 2019 halina kiingilio na linashirikisha nchi sita za Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni; Kenya,Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini na mwenyeji Tanzania.

Jana Jumamosi ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya tamasha hilo watu waliingia kwa kutumia geti la Uwanja wa Uhuru lakini leo  geti hilo limefungwa na badala yake wote wanaelekezwa kuingia geti la Uwanja wa Taifa ambapo shughuli za uzinduzi zitafanyika kisha maonyesho ya ngoma yataendelea kwenye uwanja wa Uhuru.

 

Vikundi mbalimbali vya ngoma kutoka nchi washiriki vinaendelea kutumbuiza katika jukwaa.

Tamasha hilo lilitanguliwa jana na matembezi ambapo washiriki walitembea kutoka Tandika hadi uwanja wa Taifa na kupokewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe