Upelelezi kesi ya Shamimu na mumewe wakamilika

Muktasari:

  • Upelelezi wa kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) na mkewe, Shamim Mwasha (41) umekamilika.

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) na mkewe, Shamim Mwasha (41) umekamilika.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa leo Ijumaa Machi 13, 2020 na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon wakati kesi hiyo lilipoitwa  kwa ajili ya kutajwa.

Nsembo na Shamim ambaye ni mmiliki wa blog ya 8020, wakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kinyume cha sheria.

Simon ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Rashid Chaungu kuwa upelelezi umekamilika na wanaandaa  taarifa muhimu kwa ajili ya kuziwasilisha Mahakama Kuu.

Amedai upande wa mashtaka wanaandaa taarifa muhimu kwa ajili ya kuzipeleka Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi na ufisadi kabla ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.

"Kutokana na upelelezi kukamilika tunaiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Simon.

Hakimu Chaungu  baada ya kusikiliza maelezo hayo ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 27, 2020 na washtakiwa kurudishwa  rumande kutokana na shtaka linalowakabili kutokuwa na dhamana.

Kwa mara  ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu  Mei 13, 2019.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.

Wanandoa hao wanadaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin za gramu 232.70 wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Tukio hilo wanadaiwa kulitenda Mei mosi, 2019 katika eneo la Mbezi Beach, Jijini Dar es Salaam.