Upelelezi wakwamisha kesi kigogo wa Takukuru

Friday August 23 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya kuomba na kupokea rushwa inayomkabili, Mchunguzi Mkuu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa(Takukuru) nchini Tanzania, Cosmas Batanyita( 44), bado haujakamilika.

Batanyita anakabiliwa na  mashtaka saba likiwemo la kuomba rushwa ya Sh200 milioni na kutakatisha fedha.

Leo Ijumaa, Agosti 23, 2019 Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Simon amedai mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo, anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6, 2019 kesi hiyo itakapotajwa na kuwataka upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo kwa wakati.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Advertisement

Mshtakiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Agosti 9, 2019 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 76/2019.

Kati ya mashtaka hayo saba; mashtaka matatu ni ya kushawishi rushwa, moja la kuomba na kupokea rushwa na mashtaka matatu ni ya kutakatisha fedha.

Baadhi ya mashtaka yanayomkabili Batanyita, anadaiwa Februari 9, 2019 katika eneo la Upanga, akiwa mwajiriwa wa Takukuru, alishawishi na kuomba rushwa  ya Sh200 milioni kutoka kwa Hussein Gulamal Hasham ili aweze kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji wa kodi ilivyokuwa inamkabili Hasham, wakati akijua  kuwa upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea katika Ofisi ya Takukuru.

Pia, Februari 10, 2019 katika eneo la Sabasaba, Batanyita alijipatia dola za kimarekani (USD) 20,000 kutoka Faizal  Hasham, ikiwa ni ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya ukwepaji kodi inayomkabili Hussein Hasham, wakati akijua upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa unaendelea.

Vile vile, Februari 13, 2019, katika ofisi ndogo za Takukuru zilizopo Masaki, mshtakiwa alishawishi rushwa ya dola za kimarekani (USD) 50,000 kutoka kwa Thangvelu Vall, kama ahadi ya kuharibu ushahidi katika kesi ya kukwepa kodi inayomkabili Vall.

Katika shtaka la kutakatisha fedha, Batanyita anadaiwa Februari 19, 2019 eneo la Chamazi, akiwa mwajiri wa Takukuru, alitumia fedha alizopewa kwa njia ya rushwa, kununulia kiwanja eneo la Chamazi, kwa gharama ya Sh15,8000,000, wakati akijua fedha hizo ni zao tangulizi la kosa la kuomba rushwa.

Advertisement