Utata alipo trafiki anayedaiwa kumpa mimba mwanafunzi

Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Salum Hamduni 

Moshi. Wingu limegubika mahali alipo askari wa kikosi cha Usalama Barabarani maarufu kama trafiki, anayetuhumiwa kumjaza mimba mtoto mwenye umri wa miaka 14 wa askari mwenzake.

Januari 9, Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Salum Hamduni aliliambia gazeti hili kuwa polisi huyo anashikiliwa na jeshi hilo, lakini taarifa za uhakika zimedokeza kuwa hajawahi kukamatwa.

Vyanzo mbalimbali vimeeleza kuwa Kamanda huyo aliagiza polisi huyo akamatwe na kushitakiwa kwa kosa la kubaka mwanafunzi huyo wa darasa la saba, lakini maagizo yake inadaiwa hayakufanyiwa kazi.

Siku hiyo Kamanda Hamduni alisema tayari wamemkamata polisi huyo na wanaendelea kumshikilia kwa mahojiano na ikithibitika kuwa na mahusiano watamchukulia hatua za kiutawala kwanza.

“Ni kweli tunamshikilia kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma zake na tutachukua hatua za kiutawala kwanza na kama ushahidi wa jinai utajitosheleza tutampeleka mahakamani,” alisema Kamanda huyo.

Hata hivyo, taarifa mpya zilizolifikia gazeti hili zilidai kuwa polisi huyo hakuwahi kukamatwa na polisi wala kushikiliwa, badala yake alitokomea kusikojulikana na hajaonekana kituo cha kazi zaidi ya wiki sasa.

“Hajawahi kukamatwa kama mlivyoripoti. Msala ulivyosanuka alisepa kwa kama siku tano hivi, baadaye akarudi ile kwa machale machale alipoona issue (suala) imekaa vibaya akaondoka mazima,” ilidokezwa na mtoa habari.

Gazeti hili lilipomuuliza Kamanda Hamduni jana kuhusu taarifa hizo mpya alijibu kwa kifupi tu kuwa aliagiza akamatwe na kwamba kama alitoroka kabla hajakamatwa hafahamu akaomba muda afuatilie.

Baadaye saa 10:25 alasiri mwandishi wetu alimtafuta tena kujua kama amefuatilia suala hilo, alijibu kuwa alikuwa hajapata muda wa kufuatilia kwa kuwa alikuwa ametingwa na majukumu mengine.

Vyanzo mbalimbali vimedokeza kuwa baada ya kufanyiwa vipimo vya afya yake katika hospitalini ya Serikali mjini Moshi, mtoto huyo anayesoma darasa la saba, amekutwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Habari zaidi zinadai mawasiliano ya simu baina ya polisi na mtoto huyo, yanathibitisha kuwapo kwa mahusiano ya kimapenzi kutokana na aina ya jumbe zilizokutwa katika simu ya mtoto. “Simu ya mtoto ilikutwa na messages (jumbe) za mapenzi kutoka kwa huyo polisi na mtoto alipobanwa alisema hata hiyo smartphone (simu janja) alipewa na huyo polisi,” kilidai chanzo hicho.

Mama wa mtoto huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za maadili, alisema tayari amewasilisha malalamiko kwa Kamanda wa Polisi wa mkoa, Salum Hamduni juu ya suala hilo.