Utata mpya ujenzi hospitali Ubungo

Dar es Salaam. Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo umeingia utata baada ya kuwapo madai kwamba eneo litakalojengwa hospitali hiyo ni dogo.

Hospitali hiyo inatarajia kujengwa eneo la ekari 5.5 maeneo ya Kimara Baruti jijini Dar es Salaam wakati michoro ya ujenzi wa hospitali hiyo ni ya eneo la ekari 30.

Ukweli huo ulibainika jana wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipotembelea eneo hilo na kusema kuwa ujenzi utaanza kesho na kukamilika ndani ya miezi mitatu.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic, mwongozo wa ujenzi wa hospitali za wilaya unataka zijengwe ndani ya eneo la ekari 30 tofauti na zilizotengwa ambazo ni 5.5.

Jumamosi iliyopita, Makonda alimuomba Rais John Magufuli Sh1.5 bilioni za ujenzi wa hospitali hiyo na baadaye kuibuka utata kuhusu fedha hizo baada ya Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kudai kiasi hicho cha fedha kilishapitishwa siku nyingi na Serikali ingawa Beatrice alipoulizwa jana alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita hawakuwahi kutenga kiasi hicho cha fedha na akamshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa fedha hizo.

Beatrice pia alisema ujenzi utafanyika kulingana na eneo lililopo. “Mwongozo unasema hospitali ya wilaya inapaswa kujengwa eneo la ukubwa walau ekari 30, lakini kwa mjini ni vigumu kupata eneo la ukubwa huo hapa tunafanya utaratibu wa kubadili mchoro uliopo ili kuendana na eneo tulilonalo,” alisema.

Jana, Makonda alisema ujenzi utafanyika ndani ya miezi mitatu chini ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) ambalo mkurugenzi mtendaji wake, Kanali Rajabu Mabele alisema kwa kuwa kazi hiyo imepewa kampuni ya kijeshi, itahakikisha inaikamilisha kwa muda uliopangwa na kazi itaanza mara moja baada ya kukabidhiwa mchoro.

“Rais Magufuli anataka wananchi wapate huduma haraka iwezekanavyo na ametaka hospitali hii ijengwe kwa miezi mitatu, akaniuliza nani anaweza kufanya hivyo nikamwambia hakuna mwingine zaidi ya ya JKT na kunzia kesho kivumbi kitaanza kutimka,” alisema Makonda.

Makonda pia kwa mara nyingine aliwaponda madiwani na wabunge wa upinzani kwa kutowasemea wananchi wao.

“Meya wa Ubungo, mbunge wa Kibamba na Ubungo wameshindwa kabisa kuwasemea, niwasihi tu wakati mwingine tusiwaonee haya walafi na wanaonenepa kupitia kura zenu haiwezekani wao usiku na mchana wanahangaika twitter tu mpaka najiuliza walichaguliwa huko twitter,” alisema Makonda.

Jumamosi iliyopita katika hafla ya kupokea ndege aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), mbele ya Rais Magufuli, Makonda aliwatuhumu wabunge wa upinzani mkoani Dar es Salaam kuwa hawakuwa wanawatumikia wananchi na pia ni ‘wezi’ wanaokula posho bungeni bila kufanya kazi kwa ajili ya wananchi kabla ya kumuomba mkuu huyo wa nchi kiasi hicho cha fedha, ombi ambalo liliridhiwa.

Wabunge hao ambao kwa nyakati tofauti walimjibu Makonda ni Halima Mdee (Kawe), Saed Kubenea (Ubungo) na John Mnyika (Kibamba) ambao walisema Makonda ndiye anayepaswa kusimamia maendeleo hayo.

Katika maelezo yake kuhusu Sh1.5 bilioni, Jacob alisema fedha hizo zilishatolewa na walikuwa wakisubiri ziingie katika akaunti.

Mdee kwa upande wake alisema mkoa hauwezi kuendelea kwa siasa za kudhalilisha wapinzani wakati Mnyika alisema madai ya Makonda hayana ukweli wowote bali ni propaganda za kisiasa na kumtaka alinganishe majimbo yao na yale ya CCM ya Mbagala, Ukonga, Temeke, Ilala na Segerea.

Kubenea alisema si kweli kwamba hawashiriki shughuli za maendeleo na hakwenda kupokea ndege kwa sababu alijua yatazungumzwa maneno ya kumdhalilisha.