Uwanja wa CCM Kirumba Tanzania wajaa maadhimisho ya Uhuru

Monday December 9 2019

 

By Jesse Mikofu na Sada Amir, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Usipime! Ndivyo mtu anaweza kusema kuzungumzia hamasa ya wakazi wa jiji la Mwanza nchini Tanzania na vitongoji vyake walivyojitokeza kuhudhurio maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika yanayoadhimishwa Kitaifa jijini humo.

Hamasa ya wananchi wa Mwanza na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa inaonekana kwa jinsi ambavyo wamejitokeza kuujaza uwanja wa CCM Kirumba yanakofanyika maadhimisho hayo.

Tangu saa 10:00 alfajiri ya leo Jumatatu Desemba 9, 2019, milango ya kuingilia uwanja huo ilikuwa imefunguliwa na wananchi kuanza kuingia jukwaani.

Kufikia saa 1:30 asubuhi majukwaa ya uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza zaidi ya 25, 000 yalikuwa yamejaa huku msururu mrefu wa watu wanaotaka kuingia ukiwa bado uko nje.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema wingi wa wananchi waliojitokeza umetokana na mapenzi ya Watanzania kwa Serikali na Taifa lao, hamasa na ushirikishwaji wa kila kada ya uongozi uliofanywa na kamati ya maandilizi.

“Tumetoa hamasa kupitia matangazo kwa njia mbalimbali kuanzia vyombo rasmi vya habari, mitandao ya kijamii, magari ya matangazo ya magari mitaani pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa,” amesema Mongella

Advertisement

Siyo wananchi wa kawaida pekee waliowahi uwanjani, bali hata viongozi wakuu kiwilaya, mkoa na Taifa kwa mujibu wa Katibu Tawala mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio.

Kupitia kwa tangazo lake kwa Makatibu Tawala wenzake wa mikoa ya Kanda ya Ziwa jana jioni ya Desemba 8, 2019, Kadio aliwaelekeza viongozi wote wa Serikali na taasisi zake kuhakikisha wamefika eneo la Rock city mall ifikapo saa 1:00 asubuhi ya leo tayari kwa ajili ya ukaguzi ya kuingia uwanjani.

“Viongozi wote tuwe pale Rock city mall mapema saa 1:00 asubuhi ambako tutapata kifungua kinywa, kukaguliwa na kupanda magari maalum kuingia uwanjani; atakayeshuka kwenye gari atalazimika kukaguliwa tena mlangoni,” alitoa maelekezo Kadio

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Rais wa Tanzania, John Magufuli.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Advertisement