VIDEO: Corona isipoviunganisha vyama vya siasa hakuna agenda nyingine itafanikiwa

Wednesday March 25 2020

 

By Luqman Maloto

Msomi wa uandishi wa kibunifu (creative writing), Veronica Roth wa Chuo Kikuu cha Northwester, Marekani, aliandika kwa kuhoji: “Adui yetu ni mmoja, lakini hiyo inafanya sisi tuwe marafiki?”

Ukiacha hiyuo, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice aliwahi kusema, “tunahitaji adui mmoja ili atuunganishe.” Vilevile, mwandishi James Fahy alipata kuandika kuwa “hakuna kinachoweza kuwaunganisha binadamu kama adui mmoja.”

Kwa sasa adui wa dunia ni virusi vya corona vinavyosababisha maradhi ya Covid-19. Kama dunia, kama Tanzania, ugonjwa huu ni adui wa pamoja. Na muongozo ni uleule uliotolewa na Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, takriban karne moja na robo tatu iliyopita kuwa rafiki ni yule ambaye mnachangia adui.

Vyama vyote vya siasa, kinachoshika dola (CCM) na vile ambavyo havina dola, bila shaka adui yao ni mmoja; Covid-19. Kama alivyosema Condoleezza, kuwa anahitajika adui wa pamoja ili kuwaunganisha watu, basi kwa Tanzania, hakuna kipindi vyama vya siasa vyote vinaweza kuungana kuwa na sauti moja kama sasa.

Sauti ya kupambana na corona inayoendelea kushika kasi katika mataifa mengi duniani na hapa nchini.

Hili si janga la CCM pekee kwa kuwa inaongoza dola, wala Chadema au CUF au chama chochote cha upinzani, bali kila Mtanzania, awe ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, Chauma, TLP au vyama vingine vyote.

Advertisement

Hivi kuna agenda ya kuwaunganisha wanasiasa kuliko hii ya adui wa pamoja?

Kilichokuwa chama cha matajiri na watawala wa China (Kuomintang) kilipigana vita nzito na kile cha walalahoi (Communist Party of China), sababu ilikuwa ugomvi wa madaraka.

Lakini ilipoibuka vita ya pili ya China na Japan (Sino-Japan Second War), kati ya Julai 7, 1937 na Septemba 9, 1945 Kuomintang na Communist waliungana.

Vyama hivyo vilijitathmini na kuona uadui wao si mkubwa kama ule wa Japan kwa taifa lao.

Waliunganisha majeshi yao kupigana na Japan. Vita ya Sino-Japan ilipomalizika, Kuomintang na Communist walianza tena kupigana wao kwa wao.

Kurejea kwa vita ya Wachina wenyewe kwa wenyewe ni kutimia kwa andiko lenye kuhoji kwamba kuunganishwa na adui mmoja, je, inaweza kufanya tuwe marafiki?

Ukweli ni kwamba, urafiki unasababishwa na nyenzo tofauti na zile za uadui, hivyo hata vyama vyote vikiunganishwa na agenda moja ya virusi vya corona, haimaanishi utakuwa urafiki wa moja kwa moja.

Baada ya kulishinda janga la Covid-19, kila chama kitarejea kwenye agenda yake kama ilivyokuwa kwa Kuomintang na Communist ambavyo vilirudi vitani baada ya kumshinda adui yao Japan.

Corona inatakiwa kujenga daraja la uhusiano kati ya wanasiasa, wanaharakati, watu wa dini, asasi za kiraia, wanamichezo, wasanii na makundi mengine yote ya kijamii.

Haipaswi ionekane upande mmoja watu wanazungumza haya, eneo la pili kuna ujumbe tofauti.

Septemba 2013, magaidi wa Al-Shabaab, walipovamia jengo la biashara la Westgate Mall Nairobi, Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga walijitokeza kwa pamoja kulaani tukio hilo kwa ajili ya Kenya yao.

Magaidi waliovamia Westgate walikuwa adui wa pamoja kwa Wakenya wote, vivyo hivyo kwa Uhuru na Raila. Halikuwa tukio la kutafutia mtaji wa kisiasa. Ndiyo maana pamoja na kwamba hapo awali ilidhaniwa Uhuru na Raila hawakuwa wakiiva, magaidi walipoishambulia Kenya yao waliungana kupambana nao, hawakutaka kutoa mwanya kwa maadui hao kuwagawanya, walisimama kidete kuona wanamuangamiza adui huyo. Kama alivyosema Lincoln na Condoleezza au hata Fahy ni kwamba, Uhuru na Raila walihitaji adui wa pamoja ili awaunganishe. Je, Tanzania, wanasiasa wanahitaji adui yupi mwingine zaidi ya Covid-19 ili awaunganishe wasimame pamoja?

Jibu hakuna, kwa sababu nchi inapaswa kuonekana ni moja kama ilivyo sasa. Kwa sababu kila Mtanzania ni rafiki wa Mtanzania mwenzake kwa sababu adui yao ni mmoja; Covid-19.

Na wanao wajibu wa pamoja kushirikiana kuvishinda virusi hivyo.

Hivi sasa tunahitaji kuona mwenyekiti wa CCM akizungumza lugha moja na mwenzake wa Chadema, vivyo hivyo Kiongozi wa ACT-Wazalendo, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, CUF, Chaumma, UDP, Ada-Tadea, TLP na vyama vyote.

Kila Mtanzania yupo hatarini dhidi ya virusi vya corona. Hivyo, siasa hazipaswi kuingia kwenye jambo lolote linalohusu maisha ya watu, hususan Mtanzania.

Kwa wakati huu, kauli ya Rais inatakiwa ifanane na Spika wa Bunge na hata Jaji Mkuu.

Waziri wa Afya aonekane sambamba na waziri kivuli wa afya kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani.

Wabunge wote wabebe shabaha moja, vivyo hivyo madiwani. Wazungumze na wananchi kwa lugha rahisi kuhusu namna ya kujikinga na corona.

Nchi haiwezi kuyashinda majanga kwa kutaka kuhodhi mamlaka na sauti za matamko.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alijitokeza kwenye vyombo vya habari kutangaza kuingia nchini kwa Covid-19, bila ushiriki wa waziri kivuli, wapo wanaohoji, ilikuwa bahati mbaya au makusudi kisiasa?

Kabla ya hapo, Kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe alikuwa ametangaza mikutano ya kudai Tume huru ya uchaguzi kuanzia Aprili 4, mwaka huu.

Jozi mbowe ametangaza kuahirisha mikutano hiyo hadi hapo itakapotangazwa tena, kulingana na hali itajkavyokuwa juu ya ugonjwa huo.

Ukitumia chumba chanya cha ufikiri, unaweza kubeti kuwa Mbowe angekuwa na taarifa ya Covid-19 kuingia nchini, asingetoa tamko la mikutano ya hadhara nchi nzima ili kudai Tume Huru ya Uchaguzi.

Hayo ni matokeo ya kutokuwa na uongozi shirikishi. Ummy angemshirikisha waziri mwenzake kivuli, bila shaka naye angemwambia kiongozi wake mkuu Mbowe juu ya hali hiyo na tangaza lao la mikutano lingesubirishwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitokeza kutangaza kufunga shule zote kwa mwezi mzima na kuahirisha matukio mengine yenye mkusanyiko wa kijamii bila ushiriki wa Kiongozi wa Upinzani ambaye ni Mbowe.

Inatakiwa viongozi wa kisiasa wachague matukio ya kuwagawa na yale ya kuwaunganisha.

Janga la nchi kama corona, halitakiwi kugawa watu, bali kuwaunganisha.

Corona ni janga la dunia na hakuna utani kuhusu hilo. Hoja kuwa wengi wanaopata maambukizi ya virusi hivyo hupona, haipaswi kuchukuliwa kama sentensi ya faraja kwa watu kwamba wakiambukizwa wasiogope kwa sababu watapona tu, hiyo haitoshi.

Badala yake mshikamano uwe mkubwa, elimu mahsusi iendelee kutolewa.

Watanzania wanatakiwa waujue ukweli wa ugonjwa huu kuwa unaua na unaambukiza haraka pengine kuliko ugonjwa mwingine wowote kuwahi kutokea na watu wanapaswa wawe makini.

Ni jukumu la vingozi wa kisiasa, Rais, mawaziri, wabunge na madiwani kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi.

Kama virusi hivi vya corona havitawaunganisha wanasiasa na vyama vyao kupigana vita ya pamoja, mambo mawili yatakuwa dhahiri.

Mosi, kwao masilahi ya vyama ni muhimu kuliko usalama wa wananchi na majanga wanayopitia.

Pili, hakuna agenda nyingine itakayowaunganisha.

Hivyo, jambo la msingi ni kwamba siasa ziwekwe kando mapambano yaelekezwe kwenye janga hili kwa kuwashirikisha Watanzania wote ambao wanahitaji uponyaji.

Advertisement